Mshindi wa uchaguzi wananchi wamekwishamtambua – Rais Kagame

Kampeni za uchaguzi mkuu wa urais nchini Rwanda zimeanza rasmi leo Ijumaa tarehe 14 Julai, mgombea wa kiti cha urais kupitia chama cha RPF – Inkotanyi Paul Kagame ni miongoni mwa wagombea kiti kwa muhula wa tatu.

Wagombea wengine mwaka huu 2017 ni Dr Frank Habineza, mgombea wa kiti cha urais kupitia chama cha Green Party na Mgombea wa kujitegemea Mpayimana Pillippe.

Kampeni za uchaguzi wa urais zimeanza kupamba moto

Siku ya kwanza ya kampeni za uchaguzi , mgombea wa kiti cha urais kupitia chama cha RPF-Inkotanyi Paul Kagame, ameanzia safari yake katika wilaya ya Ruhango pamoja na Nyanza jimboni kusini mwa Rwanda.

Maelfu ya wafuasi wa chama cha RPF Inkotanyi wamemiminika kwa wingi kuja kumlaki mgombea wao Paul Kagame.

Akiwahutubia wananchi, Rais Paul Kagame amesema kwamba wanaodai kuwa Rwanda hakuna demokrasia wanajidanganya, mshindi wa uchaguzi wananchi wamekwishamtambua. Rais Kagame amesema kwamba katika chama cha RPF ‘tunazidi kung’ara kama kijani kuliko chama cha Green Party . Wanaounga mkono chama cha kijani hatimaye watajiunga na RPF.

Hata hivyo, mimi nasema tu kwamba tunawashukuru kisiasa kila mmoja ana haki.’
Ameongeza kuwa zaidi ya miaka 23 iliyopita hali halisi ya nchi imeonekana kuwa ya kuridhisha lakini amewataka wananchi kuwa na imani na kujikita zaidi kuwa na maendeleo endelevu.

Naye Dr Frank Habineza mgombea kiti cha urais kupitia chama cha Green, siku ya kwanza ya kampeni zake amefanya ziara ndefu katika wilaya ya Rusizi katika tarafa ya Bugarama.

Amewaambia wafuasi wake kwamba akichaguliwa atajikita hasa kutokomeza njaa na kuimarisha teknolojia ya kisasa. Mgombea huyo wa kiti cha urais amepokewa na wananchi takriban 200 wakiwemo pia watoto.

Mgombea wa kujitegemea Mpayimana Pilippe, ameanzia zoezi hilo katika tarafa ya Nyamata, Gashora, Ruhuha na Busoro wilayani Bugesera katika jimbo la mashariki.

Akiwa pamoja na wananchi wachache, hasa wanafunzi waliokuwa wanatoka shuleni Mpayimana Pillippe amesema kwamba iwapo atachaguliwa atajikita hasa juu ya masuala ya uchumi hususan Sekta ya kilimo na kuinua zao la mpunga.

Tarehe 03 Agosti 2017 Wanyarwanda waishio nje ya Rwanda wanataraji kutumia haki yao kuchagua rais anayewafaa wakati zoezi la uchaguzi rasmi tarehe 04 Agosti 2017 itakuwa kwa wanyarwanda waishio nchini humu.


Christopher Karenzi

Changia hii habari na wenzako.

Comments

Tumia Comments