Rais wa Rwanda azuru Israel

Rais Paul Kagame alipanda mti katika msitu wa Grove of the nations uliopo mjini Jerusalem

Rais wa Rwanda Paul Kagame ameanza ziara ya siku mbili nchini israeli ambako atakutana na rais wa nchi hiyo Reuven Rivlin Jumatatu hii Julai 10.

Kabla ya kukutana na mwenyeji wake, rais Kagame atakutana na waziri mkuu wa Israeli, Benjamin Netanyahu mjini Jerusalem.

Ziara ya rais Kagame inakuja mwaka mmoja baada ya waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kuitembelea Rwanda julai 6 mwaka jana.

Mnamo mwezi Machi, rais wa Rwanda Paul Kagame alikua kiongozi wa kwanza barani Afrika kuhutubia kungamano kubwa la watu mjini Washington, nchini Marekani, ambao wanaiunga mkono serikali ya Israel, akisifu taifa hilo la Kiyahudi kuwa mfano kwa taifa lake kuzaliwa upya baada ya mauaji ya kimbari.

Rais Kagame alihudhuria mkutano wa mwaka kuhusu Israel na Marekani, ambapo amelisifu taifa hilo baada ya kufanikiwa kujiimarisha hata baada ya mauaji ya Holocaust na kuahidi Rwanda kuiunga mkono.

“Usalama wa raia ambao awali walilengwa kwa mashambulizi ili watokomee kamwe hauwezi kuwa wa kimwili tu,” alisema rais Kagame ambaye alishangiliwa na umati wa watu waliohudhuria kongamano hilo.

Nchi nyingi za Afrika zilikuwa zinaiona Israel kama muungaji mkono wa utawala wa kibaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini, lakini katika miaka ya hivi karibuni Israel imeanza kurejesha uhusiano wa kawaida wa Kidiplomasia.

Changia hii habari na wenzako.

Comments

Tumia Comments