Ivanka Trump kuwa msaidizi wa babake Marekani

Ivanka Trump (pili kulia) amesema alikuwa akifanya kazi kwa nia jema

Ivanka Trump amejiunga rasmi na serikali ya babake ambapo atahudumu kama mfanyakazi asiyelipwa, kwa mujibu wa ikulu ya White House.
Cheo chake halisi kitakuwa Msaidizi wa Rais.

Binti huyo wa rais wa Marekani amekubali shinikizo baada ya wataalamu kuhusu maadili kukosoa mpango wake wa awali wa kutaka kuhudumu katika wadhifa usio rasmi.

Bi Trump, 35, amesema amesikia "maswali ambayo baadhi ya watu wamekuwa wakiuliza kuhusu hatua yangu kumshauri rais katika nafasi yangu kama mtu binafsi".

Mumewe, Jared Kushner, ni mshauri mwandamizi wa Rais Donald Trump.
Kupitia taarifa, White House imesema ina furaha kwamba "Ivanka Trump amechukua hatua hii isiyotarajiwa katika nafasi yake kama binti wa rais".

Ivanka Trump amekuwa akihudhuria mikutano ya Trump na viongozi wa dunia
Bi Trump alisema kupitia taarifa yake kwamba amekuwa akifanya kazi "kwa nia jema na kundi la washauri wa rais White House pamoja na mshauri wake binafsi kujadili kuhusu jukumu lake".

Wataalamu kuhusu maadili walilalamika ilipobainika wiki iliyopita kwamba Bi Trump angepewa afisi White House pamoja na kibali cha usalama cha kuingia na kuondoka ikulu hiyo, bila yeye kujiunga rasmi na wahudumu wa rais.

Wakosoaji walisema kazi ya Bi Trump inafaa kufanywa rasmi ndipo aweze kudhibitiwa na sheria kuhusu uwazi wa maafisa wa serikali pamoja na maadili. Aidha, adhibitiwe na sheria kuhusu mgongano wa maslahi.

Wakili wa Bi Trump, Jamie Gorelick, amesema mteja wake atawasilisha nyaraka zifaazo za kufichua utajiri wake kwa mujibu wa sheria kuhusu maadili ya watumishi wa umma Marekani.

Changia hii habari na wenzako.

Comments

Tumia Comments