François Hollande : Ulaya haihitaji ushauri wa Trump

Rais wa Ufaransa François Hollande akosoa kauli ya Donald Trump.

Rais wa Ufaransa François Hollande amesema, Ulaya haihitaji ushauri wowote kutoka kwa rais mteule wa Marekani Donald Trump.

Kauli ya Hollande imekuja baada ya Trump kumkosoa Kansela wa Ujerumani Angela Merkel kwa kukubali wakimbizi zaidi ya Milioni moja kuingia katika nchi yake, lakini pia kupongeza hatua ya Uingereza kujiondoa katika Umoja wa Ulaya. Trump anatarajiwa kuapishwa siku ya Ijumaa.

Bw Hollande alisema hatua hiyo ya Bw Trump si ya busara.

"Ulaya haihitaji ushauri kutoka nje, kuambiwa inafaa kufanya nini," rais Hollande amesema.

Bw Trump pia amezua wasiwasi miongoni mwa viongozi wa nchi wanachama wa Umoja wa kujihami wa mataifa ya Magharibi (Nato) kwa kusema kwamba muungano huo umepitwa na wakati.

Aidha, ametishia kampuni za kuunda magari za Ujerumani kwamba ataziwekea kodi ya juu iwapo zitahamishia shughuli zake za uzalishaji Mexico.

Akihojiwa na magazeti ya Uingereza na Ujerumani, Bw Trump alisema Umoja wa Ulaya umekuwa "kimsingi chombo cha Ujerumani"

Changia hii habari na wenzako.

Comments

Tumia Comments