Viongozi zaidi ya 40 kujadili usalama leo, Mali

Rais wa Mali
Zaidi ya viongozi 40 wanatarajiwa kukutana leo kwa ajili ya mkutano wa 27 wa Africa na Ufaransa utakaojadili mambo ya Usalama na Jamii.

Rais wa Ufaransa Francois Hollande ataongoza viongozi hao kutoka nchi mbalimbali katika mji mkuu wa Mali, Bamako kwa ajili ya mkutano huo.

Unafanyika wakati ambapo kuna hali ya wasiwasi nchini humo kufuatia kuwepo kwa makundi mbalimbali ya wapiganaji.

Wiki hii pekee wanajeshi watano wa Mali wameuawa katika mripuko wa gari kaskazini mwa nchi.

Baadhi wanahoji iwapo itawezekana kwa Mali kuwa mwenyeji wa mkutano mkubwa kama huo huku ukihudhuriwa na idadi kubwa ya wajumbe wakati kukiwa na wasiwasi kuhusu hali ya usalama na hata kifedha.

Kwa mujibu wa tume ya maandalizi, rais Abdoullah Coulibaly amesema Bamako ina uwezo wa kuwa mwenyeji wa mkutano huo na itaugharamia.

’’...Mali iko tayari. Ni vigumu kutaja gharama kamili, lakini tumewekeza CFA bilioni tatu na milioni 350, zote kutoka Mali. Ni suala la kulinda hadhi yetu. Mchango wa Ufaransa ni katika matangazo tu...’’ Anasema Coulubaly

Bajeti maalumu kwa ajili ya miundombinu ya mjini Bamako kuelekea maandalizi ya mkutano kumeleta sura mpya ya mji, kama vile ujenzi uliofanyika pembezoni mwa barabara.

Balozi wa Ufaransa Frédéric Clavier anasema, mkutano huu ndio utakuwa kithibitisho kwamba Mali hivi sasa iko tayari kuhodhi mikutano mikubwa ya kimataifa tena.

Vikosi vya usalama zaidi ya elfu kumi vitatawanywa mjini Bamako kote kwa muda wote wa mkutano, kwa hiyo kila mmoja atajihisi salama akiwa mjini Bamako, angalau basi kwa hizo siku mbili ambazo viongozi watakuwa mjini.

Changia hii habari na wenzako.

Comments

Tumia Comments