Uganda yaagiza uchunguzi kuhusu raia wake aliyepigwa risasi Marekani

Maandamano mjini California nchini Marekani baada ya kuuawa kwa mtu mweusi

Serikali ya Uganda inaitaka Ubalozi wake jijini Washington DC nchini Marekani, kuchukunguza na kutoa maelezo ya kina mazingira yaliyosababisha raia wake Alfred Olango kupigwa risasi na kuuawa na polisi mjini California siku ya Jumatano.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya nje Margaret Kafeero ameliambia Gazeti la kila siku nchini Uganda la Daily Moniter kuwa, Balozi wa Uganda baada ya kufanya uchunguzi wake, itabainika wazi kilichosababisha Olango kupigwa risasi.

“Tumemwagiza Balozi wetu mjini Washington DC kutafuta ukweli wa jambo hili kwa sababu kile tunachokifahamu tu ni kuwa, raia wetu amepigwa risasi na kuuawa,”.

Polisi nchini Marekani wamekiri ni kweli, raia huyo wa Uganda mwenye umri wa miaka 30 alipigwa risasi baada ya kuonekana alitoa kitu mfukoni katika makabiliano na maafisa wa polisi.

Hata hivyo, polisi wamekiri kuwa hakuwa amebeba silaha wakati wa tukio hilo.
Baada ya tukio hilo, Wamarekani weusi na raia wengine weusi waljitokeza na kuanza kuandamana kulaani mauaji hayo.

Imebainika kuwa, Olango alikuwa ni mkimbizi kutoka nchini Uganda lakini pia alikuwa anasumbuliwa na maradhi ya akili, suala ambalo pia huenda lilichangia makabiliano yake na polisi.

Polisi wamesisitiza kuwa, walimwagiza atoe mikono mifukoni mwa suruali yake lakini akatoa kitu ambacho kimebainika kuwa sigara ya kieletroniki.

Marekani imeendelea kushuhudia vifo vya Wamarekani na wahamiaji haramu mikononi mwa polisi wazungu.

Changia hii habari na wenzako.

Comments

Tumia Comments