Uchaguzi nchini Somalia waanza huku Al Shabab ikitishia kuusambaratisha

Wabunge wa bunge la Somalia wakishiriki katika upigaji kura katika siku zilizopita mjini Mogadishus.

Somalia imeanza zoezi la kuwateua wabunge 275, zoezi ambalo linatarajiwa kumalizika tarehe 10 mwezi Oktoba.

Wagombea mbalimbali wamekuwa wakionekana mjini Mogadishu, Baidoa na Kismayu wakishiriki kwenye kampeni kuomba uungwaji mkono ili kupata nafasi ya kuingia bungeni.

Uteuzi wa wabunge hao wapya unafanywa na wajumbe 51 ambao ni viongozi wa dini, watu wenye ushawishi katika jamii na wazee kutoka koo mbalimbali nchini humo.

Kuna wagombea 14,025 wanaotafuta nafasi ya kuingia bungeni.
Zoezi hili linaloungwa mkono na Jumuiya ya Kimataifa, linashuhudia pingamizi kubwa kutoka kwa kundi la kigaidi la Al Shabab.

Msemaji wa kundi hilo ambalo linataka kuongoza nchi hiyo Sheikh Ali Mohamoud Rage amesema wapiganaji wake watahakikisha kuwa wanaharibu zoezi hilo.

Licha ya tishio hili, jeshi la Umoja wa Afrika linalopambana na kundi hilo AMISOM, limetoa hakikisho kuwa litafanya kila kilicho ndani ya uwezo wao ili Uchaguzi huo ufanikiwe.

Wabunge watakaokuwa wameteuliwa watakuwa na kazi kubwa ya kumchagua rais wa nchi yao mwezi Oktoba.

Rais wa sasa Hassan Sheikh Mohamud anatetea nafasi yake lakini anakabiliwa na ushindani kutoka kwa wagombea wengine sita akiwemo mwanamke mmoja.

Changia hii habari na wenzako.

Comments

Tumia Comments