Raia wa Zimbabwe waandamana kupinga utawala wa Mugabe nje ya ofisi za UN

Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe, akihutubia baraza la umoja wa Mataifa kwenye moja ya mikutano aliyowahi kuhudhuriaUN

Wanaharakati na wakosoaji wa Serikali ya Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe, wameanza maandamano ya mfululizo nje ya makao makuu ya umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani wakiongeza shinikizo kwa kiongozi huyo kuondoka madarakani.

Rais Mugabe ambaye ametawala taifa la Zimbabwe kwa zaidi ya miongo mitatu, hivi karibuni amekuwa kwenye shinikizo kubwa toka kwa wanaharakati na viongozi wa upinzani wanaopinga utawala wake, kwa kile wanachosema ameshindwa kuongoza.

Maandamano haya yanafanyika wakati huu ambapo viongozi wa dunia wakianza kuwasili jijini New York, kuhudhuria mkutano wa 71 wa baraza la Umoja wa Mataifa uliong’oa nanga kuanzia mwishoni mwa juma.

Kwenye maandamano hayo ambayo yamewakutanisha pamoja makundi mbalimbali likiwemo vuguvugu la kundi la “This Flag” linaloongozwa na mchungaji maarufu Evans Mawarire, raia wa Zimbabwe sasa wanafanya harakati zao hata nje ya taifa lao, wakitaka mabadiliko ya kisiasa na kuomba msaada kutoka Jumuiya ya Kimataifa.

Miongoni mwa waandamanaji hao yumo kaka wa Itai Dzamara, mwandishi wa habari na mwanaharakati wa demokrasia, ambaye bado hajulikani alipo baada ya kudaiwa kutekwa nyara miezi 18 iliyopita mjini Harare.

Vinara wa maandamano haya wamesema kuwa,lengo lao ni kutaka kuionesha Jumuiya ya Kimataifa kuwa, imetosha ! Na kwamba wanataka kuona kuna kuwa na mabadiliko ya kiutawala ifikapo mwaka 2018 na kuendelea.

Wanaharakati hao wamesema kuwa kwasasa hawafahamu ikiwa Itai yuko mzima ama ameshauawa kwakuwa tayari zaidi ya miezi 18 imeshapita toka atoweke, ambapo kabla ya kutekwa kwake, alisimama peke yake kwenye viwanja vya makao makuu ya umoja wa Afrika mjini Addis Ababa na kumtaka Rais Mugabe aondoke madarakani.

Wananchi hao wanasema kuwa, wamechoshwa na utawala wa Rais Mugabe, na kwamba lengo lao ni kuhakikisha kiongozi huyo anaondoka madarakani ikiwezekana hata kabla ya muhula wake kutamatika.

Rais Mugabe anatarajiwa kulihutubia baraza la umoja wa Mataifa Jumatano ya wiki hii, ambapo kama ilivyokawaida yake, anatarajiwa kuyakashifu mataifa ya magharibi kwa kupandikiza dhana ya uchochezi nchini mwake pamoja na vikwazo ilivyowekewa.

Wachambuzi wa mambo wanaona kuwa maandamano haya licha ya kuwa yatakuwa na mchango kidogo kufikia malengo, lakini ujumbe utakuwa umefika hasa kwa mataifa ambayo yanakosoa utawala wa Rais Mugabe.

Changia hii habari na wenzako.

Comments

Tumia Comments