Hatma ya mvutano kati ya Serikali na upinzani Tanzania kujulikana Sept Mosi

Wananchi wakiwa katika moja ya mikutano ya kampeni nchini Tanzania
Ikiwa ni saa chache tu zimebaki kabla ya chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, CHADEMA kuanza operesheni yake ya nchi nzima iliyopewa jina la “UKUTA” Septemba Mosi mwaka huu, wananchi wengi bado wana hofu ikiwa maandamano hayo ya upinzani yatafanyika au la.

Upinzani nchini Tanzania umeshikilia msimamo wake wa kufanya maandamano ya nchi nzima Septemba Mosi licha ya zuio la Polisi na Serikali.

Viongozi wa upinzani wanasisitiza kuwa hawawezi kufungwa mdomo wa Serikali katika kufikisha ujumbe wao kwa wananchi, kuwaeleza kile ambacho wanasema kuanza kuminywa kwa Demokrasia na Serikali ya awamu ya tano.

Mwishoni mwa juma lililopita na mwanzoni mwa juma hili, viongozi wa juu wa chama hicho cha upinzani walikamatwa na Polisi wakati wakiwa wanafanya vikao vyao vya ndani, ambapo walihojiwa kwa saa kadhaa kabla ya kuachiwa kwa masharti.

Jeshi la Polisi nchini Tanzania linasema limejipanga kuhakikisha nchi inakuwa salama, na kuwatoa hofu wananchi kuhusu uwezekano wa kufanyika kwa maandamano hayo, likisema halitakubali watu wachache wavunje amani ya nchi kwa kufanya maandamano yaliyokatazwa.

Juma moja lililopita, jeshi la Polisi lilifanya mazoezi iliyosema yalikuwa ni mazoezi ya kawaida ya jeshi hilo katika kupima weledi wa vijana wao kukabiliana na maandamano, mazoezi ambayo upinzani uliyatafsiri kama kitisho kwa wananchi.

Kamati kuu ya chama cha upinzani imeendelea kukutana na Jumatano ya wiki hii wanatarajiwa kutoa kauli na msimamo wao wa mwisho ikiwa watafanya maandamano siku ya Alhamisi, September Mosi mwaka huu ama wata ahirisha maandamano hayo.

Viongozi wa dini pamoja na msajili wa vyama vya siasa waliingilia kati mvutano huu, ambapo walikubaliana kukutana na viongozi wa vyama vya siasa kujaribu kuzungumzia sintofahamu iliyojitokeza.

Wananchi wanasubiri kujua hatma ya maandamano haya, huku wengi wakionesha kuwa na hofu ya kutokea kwa vurugu ikiwa upinzani utaendelea mbele na kufanya maandamano ambayo tayari wadadisi wa mambo wanasema huenda yakwa ya vurugu, huku baadhi wakitofautiana.

Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli, bado hajalegeza msimamo wake kuhusu marufuku aliyotangaza kwa vyama vya siasa kufanyua mikutano ya kisiasa hadi mwaka 2020, huku akiruhusu mikutano ya wabunge waliochaguliwa kwenye maeneo yao.

Changia hii habari na wenzako.

Comments

Tumia Comments