Upinzani Tanzania kuendelea na maandamano yao, waomba Jumuiya ya Kimataifa kuingilia

Mwanasheria mkuu wa chama cha upinzani nchini Tanzania, CHADEMA
Chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, CHADEMA, kimesisitiza kuwa maandamano yaliyopangwa kufanyika September Mosi mwaka huu, yako pale pale na kwamba hawana nia ya kusitisha mkakati wao.

Wakizungumza jijini Dar es Salamaa, Alhamisi ya wiki hii, mwanasheria mkuu wa chama hicho, Tundu Lissu, amesema kuwa, chama chao hakijabadili mpango wa kufanya maandamano tarehe mosi ya mwezi ujao, na kuwataka wafuasi wao kujiandaa.

Lissu amesema wao kama viongozi wa juu wa chama, hawawezi kukaa kimya huku wakitazama demokrasia ikiendelea kuminywa na utawala wa awamu ya tano,
ambao wanasema umeamua kufanya masuala yake kwa kutumia mabavu.
Amesema zuio la Polisi kuhusu kufanya mikutano yao ya ndani linaenda kinyume na sheria za nchi na kwamba wao kama chama wataendelea na mikutano yao ambayo tayari ilikuwa imepangwa toka awali.

Lissu amesisitiza kuwa kitendo kinachofanywa na Serikali hakikubaliki na ndio maana wao kama wapigania demokrasia wa taifa hilo, hawatafumbia macho suala hili lipite.

Kuhusu madai ya Polisi kuwa tukio la kuuawa kwa askari wake wanne Usiku wa kuamkia Jumatano ya Agosti 24 lilipangwa kisiasa, chama cah CHADEMA kimekanusha kuhusika kwa vyovyote vile katika shambulio hilo na kuwataka Polisi kutimiza majukumu yao kuwasaka wahusika.

Kwa upande wake makamu mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Abdalah Safari, amesema anashangazwa kuona yeye kama miongoni mwa waliopigania demokrasia ya taifa hilo, sasa inaingia dosari kwa kile alichosema ni kama inamwagiwa maji ya baridi na viongozi walioko madarakani.

Profesa Safari ameongeza kuwa, kitendo cha vyama vya siasa kunyimwa haki ya kufanya mikutano ya hadhara ambayo imeanishwa wazi kwenye sheria ya vyama vya siasa, inaendana kinyume kabisa na katiba ya nchi, huku jeshi la Polisi likitumiwa isivyo sahihi kutekeleza amri ambazo ziko nje ya mipaka yao.

Kwa upande wake Lawrance Masha aliyewahi wakati fulani kuwa waziri wa mambo ya ndani ya nchi, amesema mazoezi yaliyofanywa hivi karibuni na jeshi la Polisi, yalilenga kuwatengenezea wananchi hofu ili wasijitokeze katika kuunga mkono harakati zao za kupigania demokrasia.

Chama hicho kimetoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa kuingilia kati kile kianchoshuhudiwa hivi sasa nchini Tanzania, na kuitaka kuweka shinikizo kwa Serikali kuheshimu haki za binadamu na uhuru wa watu kukusanyika kama sheria za nchik zinavyoruhusu.

Haya yote yanajiri baada ya Serikali kupitia agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli, kupiga marufuku mikutano yote ya kisiasa kwa kile alichosema huu sio wakati wa kufanya siasa na badala yake akataka mikutano ifanyike kwenye majimbo ambako wabunge walichaguliwa na wananchi.

Jeshi la Polisi nchini Tanzania, limeonya kuhusu kufanyika kwa maandamano ya upinzani tarehe Mosi ya mwezi ujao, na kuapa kuwashughulikia wale wote watakaojihusisha na maandamano hayo.

Changia hii habari na wenzako.

Comments

Tumia Comments