Rwanda yatoa salamu za rambirambi kwa Italia

Idadi ya watu waliofariki kutokana na tetemeko la ardhi katikati mwa Italia mapema Jumatano imefika 247 huku manusura wakiendelea kutafutwa kama BBC inavyosema.
Maafisa wa uokoaji wanaendelea na juhudi za kutafuta manusura na miili kwenye vifusi.

Tetemeko hilo la nguvu ya 6.2 katika vipimo vya Richter liliharibu vibaya miji ya Amatrice, Accumoli na Pescara del Tronto ambapo watu wengi walifariki.

Akitumia ukurasa wake wa twitter, Louse Mushikiwabo, waziri wa mashauri ya kigeni na ushirikiano na pia msemaji wa serikali ya Rwanda, katika ujumbe wake alimuambia balozi Forana wa Italia kwamba Rwanda na marafiki wa Italia wanaoishi nchini Rwanda wanawaunga mkono wananchi wa Italia katika hii hali ya dhiki.

‘’ ndugu Balozi D. Forna, serikali ya Rwanda na marafiki wa Italia nchini Rwanda tumesikitishwa na vifo vilivyosababishwa na tetemeko la ardhi, sisi tunawatakia nyinyi na familia zenu kuwa na nguvu.’’ Mushikiwabo aliandika.

Maafisa wa uokoaji waliendelea na juhudi za kuwatafuta manusura usiku, lakini wakati mmoja walitatizwa na mitetemeko mingine iliyotokea na kutikisa majumba yaliyosalia yakiwa bado wima.

Eneo lililokumbwa na tetemeko hilo ni milimani katika majimbo ya Umbria, Lazio na Marche.

Kitovu cha tetemeko hilo kilikuwa karibu na Norcia, kilomita 170 kaskazini magharibi mwa mji mkuu Roma.

Mahema yamewekwa kuwasaidia watu walioachwa bila makao.

Changia hii habari na wenzako.

Comments

Tumia Comments