Wachezaji 10 bora walioanza vyema Ligi kuu ya Uingereza na klabu zao mpya

KATIKA suala la uhamisho wa wachezaji kutoka klabu moja kwenda nyingine mara kadhaa kunakuwa na aina tatu zinazomtokea mchezaji.

Kuanza vyema kikosini na kung’ara moja kwa moja, kuanza vibaya na baada ya muda mfupi kuzoea mazingira mageni kisha mchezaji anakuwa bora zaidi na kundi la tatu ni kudorora kabisa na kupotea kwenye soka la kiushindani.

10) Alvaro Negredo (Middlesbrough)

Ni straika wa zamani wa Manchester City aliyetimkia Valencia 2014. Msimu huu amerejea kwa mara nyingine Ligi Kuu England akiwa na kikosi cha Middlesbrough. Negredo alianza vyema kuitumikia klabu yake hiyo akiingia kimiani kwa mpira wa ‘free kick’ safi uliozaa bao pekee na kuifanya Middlesbrough kwenda sare ya 1-1 dhidi ya Stoke City. Mhispania huyo mwenye umri wa miaka 30, wastani wake wa kufunga ni 7.42.

9) Idrissa Gueye (Everton)

Given ni straika aliyesajiliwa msimu huu na klabu ya Everton kwa pauni milioni 7, akitokea Aston Villa. Msenegali huyo alionyesha kiwango cha kuvutia sana eneo la kiungo, akisaidiana na mfungaji wa bao, Rose Barkley. Gueye ambaye anacheza nafasi ya kiungo mkabaji, alitimiza majukumu yake ya kukaba vizuri kwa wakati, huku akipokonya mipira ambapo kwa sasa anatazamwa kama ‘injini’ mpya ndani ya dimba la Goodison Park.

8) Fernando Llorente (Swansea City)

Swansea City ilikuwa na pengo la straika Bafetimbi Gomis, aliyeondoka mwaka 2014 kwenda nchini Ufaransa, kukipiga kwa mkopo katika klabu ya Marseille.

Pia kulikuwa na pengo jingine la winga wa kushoto, Andre Ayew, lakini usajili wa Fernando Llorente akisaidiana na ingizo jingine jipya, Borja Baston, ulionekana huenda utaendana na kasi ya Ligi Kuu England.

Llorente alionekana kuwa mwiba kwa mabeki hasa anapofika eneo la hatari la adui. Ni mchezaji pekee aliyepiga mashuti mengi kuelekea langoni akifanya hivyo mara sita, ambapo wastani wake wa kuchana nyavu ni 7.51.

7) George Friend (Middlesbrough)

George Friend mwenye umri wa miaka 28 anayecheza beki ya kushoto ni mzuri kuanzisha mashambulizi kutokea pembeni, huku pia akiwa na uwezo mkubwa wa kukokota mpira. Anatajwa kama beki wa kipekee aliyeweka rekodi katika mchezo wa kwanza, akikokota mpira mara nyingi kuliko beki mwingine yeyote, huku akizuia mashambulizi ‘interceptions’ hatari mara nne. Ubora wake huo uliiwezesha Swansea kushinda bao 1-0 mbele ya Burnley FC.

6) Andros Townsend (Crystal Palace)

Licha ya timu yake hiyo mpya ya Crystal Palace kupoteza mchezo wa kwanza wa ligi kwa kuchakazwa bao 1-0 na West Brom Agost 14, Andros Townsend, alionyesha ubora wake uwanjani akitokea winga ya kulia, akipiga jumla ya mashuti sita na kuzuia mashambulizi ‘interceptions’ mara tisa.

5) Nathan Redmond (Southampton)

Kocha mpya wa Southampton, Claude Puel, anaamini fowadi wake huyo aliyemvuta kutoka Norwich, atakuwa msaada mkubwa kikosini kwake hasa kutokana na kutumia mfumo wake anaoupenda wa 4-3-1-2.

Redmond alianza kufungua akaunti ya mabao katika dimba la St Mary katika mchezo uliomalizika kwa sare ya bao 1-1 mbele ya Watford.

4) Gaston Ramirez (Middlesbrough)

Baada ya kupata uhamisho wa kudumu wa majira haya ya kiangazi katika klabu ya Middlesbrough, akitokea Southampton, Gaston Ramirez mwenye umri wa miaka 25, ameonyesha kwamba anafaa kuendelea kuwepo hapo.

Muuruguay huyo alionyesha soka la kiwango cha juu akitoa pasi ya bao kwa Negredo, katika dimba la Riverside, walipokutana na Stoke City.

Vile vile ana uwezo wa kupiga pasi sahihi kwenda kwa mlengwa ambapo ana wastani wa 8.21 kuwaokotesha makipa mpira nyavuni.

3) Adama Diomande (Hull City)

Adama Diomande ambaye ni raia wa Norway, Hull City inakuwa timu yake ya saba kuichezea tangu aanze kucheza soka la ushindani ngazi za juu, huku pia England likiwa ni taifa lake la tatu kucheza katika ligi kubwa duniani.

Mara yake ya kwanza tu kushuka uwanjani mwishoni mwa wiki iliyopita, alicheza vyema na kufanikiwa kuwazuia vilivyo mabingwa watetezi Leicester City kupata matokeo chanya.

Diomande, 26, alikuwa shupavu pia katika kupokonya, kukokota mipira mara sita na kucheza faulo nne.

2) Zlatan Ibrahimovic (Manchester United)

Zlatan Ibrahimovic anawekwa kwenye orodha ya nyota wa daraja la juu kabisa katika soka pamoja na umri wake mkubwa wa miaka 34, ambapo ameweza kudhihirisha ubora wake katika kupachika mabao.

Achana na bao lake la ushindi lililoiwezesha Manchester United kutwaa Ngao ya Jamii mbele ya Mabingwa watetezi Leicester City, Msweden huyo alianza vyema mbio za kufukuzia kiatu cha dhahabu kwa kufunga bao katika mchezo wa kwanza wa ligi dhidi ya Bournemouth.

Mkali huyo aliyesajiliwa na Mashetani Wekundu, Manchester United kama mchezaji huru akitoka Paris Saint Germain (PSG) ya Ufaransa, wastani wake wa kufunga ni 8.28.

1) Sadio Mane (Liverpool)

Msenegali aliyefanikiwa kusajiliwa na Majogoo wa London, Liverpool baada ya kushinda vita ya timu nyingine kubwa zilizokuwa zikimfukuzia winga huyo wakiwemo mahasimu wao, Manchester United alikuwa ni miongoni mwa wafungaji wa mabao 4-3 katika viunga vya Emirates.

Mane aliitesa sana ngome ya Arsenal kwa kiasi kikubwa hali iliyomfanya kuchezewa faulo zaidi ya nne, akikokota mpira mara sita, ni aina ya wachezaji wanyumbulifu na wabunifu wanaoendana na mfumo wa kocha Mjerumani, Jurgen Klopp, huku akitajwa kama mchezaji tegemeo siku za usoni Anflied.

Martin Hubert IKURAMUTSE

Changia hii habari na wenzako.

Comments

Tumia Comments