Kuingia katika ndoa si kama kuingia katika duka la nguo

Katika sherehe nyingi za harusi unazoenda kuhudhuria, wapo wanaoolewa wakiwa na furaha ya kuanzisha maisha kamili na wale wanaowapenda. Pia wapo wanaoingia katika ndoa kwa sababu walitamani kuolewa. Umenielewa hapo ?

Japo mambo haya yalikuwapo toka zamani, ila ni ukweli ulio wazi kuwa siku hizi yamekuwa na utawala zaidi. Zamani athari za ndoa hizi hazikuwa kubwa kwa sababu mabinti wa zama hizo mbali na kushiba maadili na uoga uliofanya wasithubutu kufuata misimamo ya hisia zao ila pia hali ya zama hizo ilikuwa tofauti sana na sasa.

Mabinti baada ya kuwa na kina fulani kwa muda fulani wanahitaji ndoa. Hawana mapenzi ya kweli wala hawawahitaji kwa dhati katika nafsi zao. Kila siku kutakuwa na ugomvi ama dharau katika nyumba yao. Ni ndoa gani inayofungwa bila kiunganishi cha upendo ikawa na amani na utulivu ?

Kwa kuwa hawana hisia za kweli na wahusika, wengi wamejikuta njia panda na hatimaye kuzaa watoto na watu wasiowahitaji katika maisha yao. Ndoa ni suala la kifamilia, ni suala la maisha yako pia ni suala linalomshirikisha Muumba wako. Katika maamuzi yako katika hili acha kukurupuka.

Ndoa yako inaweza kukupa amani au huzuni kubwa katika maisha yako. Wangapi kabla ya ndoa walikuwa wanene ila sasa hivi wamebaki kama moja ? Si kwa sababu ya ‘diet’ wala mazoezi ila shida na mabalaa ya ndoa zao yamewafanya kuwa hivyo.

Tumeona wengi walioingia katika ndoa na kisha tukaona wakizidi kuimarika kiafya,
kihali na kimandeleo. Pia wapo wengi walioingia katika ndoa na kugeuka kuwa watu wa misongo ya mwazo, waliofubaa wajihi wao na kuyumba sana kiuchumi. Unapofikiria ndoa, fikiria katika namna pana zaidi ya starehe ya kitandani.

Tulia, jione una thamani. Hakuna jambo linalotokea bila ya sababu. Ukiwa mstahamilivu na mwingi wa subira, kila kitu kwako kitawezekana ila kama ukiwa na pupa, utaingia katika ndoa mapema ila pia utaumia zaidi na pengine kutoka mapema zaidi huku ukiwa huna hamu tena ya ndoa na sifa yako kuwa imechafuka.


Martin Hubert IKURAMUTSE

Changia hii habari na wenzako.

Comments

Tumia Comments