Rais Magufuli awataka Watanzania kuilinda amani

Rais Dkt John Magufuli amewataka watanzania kuilinda amani ya nchi na kusisitiza ikipotea hakuna atakayefaidika.

Ameyasema hayo Jumatano hii wilayani Sengerema, mkoani Mwanza katika ziara yake ya siku mbili mkoani humo .

“Palipo na amani ndipo kila kitu kitafanyika hapa tulipo kaa tupo vyama mbalimbali, tupo dini mbalimbali, lakini wote tumekaa pamoja ni kwasababu amani ipo na imejengwa chini ya misingi ya waasisi wetu Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere,”
alisema Dkt Magufuli.

Rais huyo wa awamu ya tano, aliongeza, “Tanzania tuna makabila zaida ya 121 lakini wala hatuulizani wewe ni kabila gani, Rwanda pale na nchi zingine kwenye mwaka 1994 watu waliuana kwasababu wewe ni Mrutu yule ni mtusi na wote wanazungumza lugha moja tofauti yake ni pua,” aliongeza.

Alisisitiza kwa kutoa mfano huo wa Rwanda kuwa walishindwa kuilinda amani kuna nchi nyingi zimesambaratika. “Sasa hivi, kuna nchi zilizo kuwa na maendeleo makubwa sana katika Afrika na sioni aibu kutoa mfano, nchi kama Libya, Libya ilikuwa mtu ukienda kuposa unapewa dola zaa kulipa mahali na unatafutiwa nyumba ya kukaa.”

Aidha aliendelea kusema kuwa Libya wanauana kila siku kwa sababu hawakuitunza amani yao. “Kuna sehemu nyingi tumekuwa tukisikia kwenye taarifa ya habari kuwa watu wakiuana kila siku.”

“Watu wanaochafua amani anaweza hata akawa ndugu yako, watu wanaweza wakatumia dini, wakatumia kabila hata siasa na wakati mwingine wanaweza wakatumiwa au wakatumia.”

“Nawaomba watanzania na wanasengerema kwa ujumla tuitunze amani yetu, amani ikipotea hakuna atakayefaidika kuna wengine watasema tutafanya hivi tutafanya vile,”alisisitiza.

“Naomba msije mkadanganywa wala mkadanganyika, simamieni amani yetu vyama vyetu peleka nyuma peleka Tanzania kwanza, dini zetu peleka nyuma weka Tanzania kwanza, makabila yetu weka nyuma peleka Tanzania kwanza, palipo na amani ndipo utakavyofanya biashara yako vizuri na kwa amani.”

Changia hii habari na wenzako.

Comments

Tumia Comments