Kabila azuru Uganda

Rais wa DRC, Joseph Kabila akiwa na mwenzake wa Uganda, Yoweri Museveni.

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Josephu Kabila, yuko nchini Uganda kwa ziara ya kikazi ambapo amekutana na mwenyeji wake Rais Yoweri Kaguta Museveni.

Duru kutoka kwenye Serikali ya Kinshasa, zinasema kuwa ziara ya Rais Kabila nchini Uganda, imelenga kujaribu kuishawishi nchi hiyo, kuzidisha mashambulizi dhidi ya wapiganaji wa ADF NALU wanaopigana mashariki mwa DRC.

Wapiganaji wa ADFU NALU ambao asili yao ni kutoka nchini Uganda, wamekuwa wakipigana mashariki mwa nchi ya DRC kwenye mji wa Beni, ambako wanaripotiwa kutekeleza vitendo vya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.

Rais Joseph Kabila, anatarajiwa kumueleza Rais Museveni hatua ambayo jeshi la nchi yake limefikia katika vita dhidi ya ADF NALU na pengine kumshawishi kiongozi mwenzake kusaidia makabiliano dhidi ya kundi hilo.

Rais Kabila alitokea mjini Goma, ambako alikutana na wananchi wa eneo hilo na kuwahakikishia usalama, wakati huu jeshi la Serikali FARDC likiendesha operesheni ya pamoja na vikosi vya umoja wa Mataifa, MONUSCO.

Wananchi wa eneo la mashariki mwa DRC wameonesha kuwa na matumaini kuhusu ziara ya Rais Kabila nchini Uganda, ambapo wanaharakati wa mashirika ya kiraia wanasema ni imani yao kuwa Rais Kabila na Museveni watakubaliana kuhusu njia za kulikabili kundi hilo.

Changia hii habari na wenzako.

Comments

Tumia Comments