Mameya wawili Rwanda wahukumiwa

tangu kushoto Octavien Ngenzi na Tito
Mameya wawili wa zamani wa Rwanda wamehukumiwa kifungo cha maisha jela mjini Paris kutokana na kuhusika kwao na mauaji ya kimbari yaliyotekelezwa mwaka 1994.

Octavio Ngenzi na Tito Barahira walikutwa na hatia ya uhalifu dhidi ya binadamu na pia kusaidia na kupanga mauaji ya watu wa jamii ya watutsi katika vijiji vyao upande wa Mashariki mwa Rwanda.

Ni kesi ya pili kuamuliwa nchini Ufaransa dhidi ya watu wanaotuhumiwa kushiriki katika mauaji hayo ya kimbari.Octavien Ngezi alikuwa Meya wa Kabarondo. Tito Barahira alikuwa mtangulizi wake katika nafasi hiyo.

Katika hukumu ndefu na ya kuchosha, wanasheria wa Ufaransa walifikia muafaka kuwa wanaume hawa wawili walichangia pakubwa katika mauaji ya kimbari katika eneo la Kabarondo mwezi wa April mwaka 1994.

Katika mauaji yaliyotekelezwa kwa ukatili mkubwa mamia ya wanaume, wanawake na watoto walichinjwa baada ya kutafuta hifadhi katika kanisa la kijiji.

Kwa miaka 22 Kesi ilikuwa ikiegemea katika ushahidi wa watu walioshuhudia, na upande wa utetezi ulijitetea kwa kusema kuwa baada ya kipindi hicho kirefu kumbukumbu zilikuwa si za kuaminika tena na kwa hivyo ushahidi huo si wa kufaa.
Watuhumiwa hao wawili muda wote waliendelea kusema kuwa walikuwa watazamaji wa tukio ambalo wasingeweza kusaidia lolote katika kilichotokea.

Lakini mwisho mahakama ikahukumu kuwa walishiriki katika kupanga na kutekeleza mauaji yaliyolenga kumaliza watu wote wa jamii ya watutsi.

Sheria za ufaransa zinazipa haki mahakama za ufaransa kuhukumu makosa dhidi ya ubinadamu na mauaji ya kimbari hata kama makosa hayo yalitendeka nje ya ufaransa.

Miaka miwili iliyopita sheria hii ilitumika kwa mara ya kwanza kwa kumuhukumu mnyarwanda mwingine Pascal Simbikangwa afisa wa usalama ambaye naye alikutwa na hatia ya kushiriki katika mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi mwaka wa 1994.

Changia hii habari na wenzako.

Comments

Tumia Comments