Papa Wemba : Nguli wa muziki wa Afrika aliyefariki dunia kazini, mfahamu zaidi

Ilikuwa ni Kusini mwa Congo (Zaire kuanzia 1965 hadi 1997) kisha kuwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo) kwenye mkoa wa Kasai ambapo Papa Wemba alizaliwa mwaka 1949.
Jina lake halisi ni Shungu Wembadio Pene Kikumba, lakini alipewa jina Papa kwasababu alikuwa mtoto wa kwanza.

Alipokuwa mtoto mchanga, familia yake ilihamia Leopoldville, mji mkuu wa nchi hiyo kipindi cha utawala wa Wabelgiji. Baba yake alikuwa mwanajeshi mstaafu aliyepigana vita vikuu vya pili vya dunia kabla ya kuwa mwindaji.
Mama yake alikuwa muombolezaji mazishi anayelipwa. Kwa kwenda naye mara kwa mara kwenye shughuli hizo, mama yake alimtambulisha kwenye muziki ambao alijikuta akiupenda.

Hata hivyo baba yake alipinga vikali mwanae kuwa mwanamuziki kwasababu alitaka aje kuwa mwandishi wa habari au mwanasheria.

Baba yake Papa Wemba alifariki mwaka 1966. Hakuchelewa na aliamua kuingia kwenye muziki moja kwa moja. Alianza kuimba kwenye kwaya ya kanisa la Mtakatifu Joseph na akatengeneza sauti yake ya juu iliyokuwa moja ya tofauti kubwa na waimbaji wengine.

Katika miaka ya 60, aliimba na vikundi mbalimbali katika mji huo mkuu ambao wakati huo ulibadilishwa jina na kuitwa Kinshasa baada ya kupata uhuru. Kama vijana wengi wa enzi hizo, Papa Wemba alivutiwa na muziki wa Kimarekani na kubadilisha jina lake kuwa Jules Presley.

Mwaka 1969 alikuwa sehemu ya waimbaji waliozalisha kundi lililotamba miaka ya 70, Zaiko Langa Langa. Kundi hilo lilipata umaarufu mapema kwa vijana ambao walianza kuhisi muziki asili wa rhumba ulikuwa wa pole pole mno na uliopitwa na wakati.

Tangu miaka 50, Afrika nzima ilikuwa ikicheza mtindo huu uliokuzwa na Joseph Kabasele na kisha Franco miaka ya 60. Zaiko Langa Langa walikuja na muziki uliochangamka zaidi na Papa Wemba akang’ara mapema na kuliongoza kundi.

Mwaka 1975, baada ya kupata jina, Papa Wemba aliondoka kwenye kundi hilo na kuanzisha kundi lake, Isifi Lokole. Isifi lilikuwa ni kifupi cha Institut de Savoir Idealogique pour la Formation des Idoles (Institute of Ideological Knowledge for the Training of Idols) na Lokole ni jina la kifaa cha muziki kutoka Kasai.

Mwaka 1977 Papa Wemba alianzisha Viva La Musica, kundi lililokuwa na wanamuziki takriban 15 ambalo pamoja na mabadiliko ya hapa na pale bado lipo.
Ukubwa wake haukuwa kwenye muziki tu. kwenye viunga vya Kinshasa, Papa Wemba alitengeneza kijiji alichokipa jina “Kijiji cha Molokai” na kujiweka kama kiongozi mkuu.

Ndani ya kijiji hicho alianzisha uvaaji wake. Wakazi wake walitakiwa kuongea kwa namna tofauti, kutembea kivyao. Ulikuwa ni mji uliokuwa ndani ya mji na wenye sheria zake.
Mwaka 1979 aliimba kwa miezi michache na bendi ya Tabu Ley, Afrisa International Orchestra of Tabu Ley na kisha mwaka 1980, alifanya ziara ya Afrika akiwa na santuri ya Analengo iliyouza nakala 60,000.
Miaka ya 80 Papa Wemba aliingia mkataba mnono na lebo ya Visa 80 ya Luambo Makiadi, maarufu kama Franco.

Akiwa na safari nyingi za Ulaya alikokuwa akirekodi nyimbo zake, Papa Wemba aling’ara kwa fashion zake na kuwa prince wa jamii ya SAPE (Societe des Ambianceurs et des Personnes Elegantes – Society of Posers and Elegant People).
Mwaka 1983, alienda Ulaya alikokaa kwa miezi minane na kuliacha kundi lake Viva La Musica, chini ya uongozi wa mke wake, Amazon. Kundi hilo liliyumba kutokana na wanamuziki kulipwa ujira kidogo.

Alirejea July 1984 na kulirejesha tena kundi lake kwenye chati. Aliamua kuhamia Ulaya mwaka 1986 baada ya kufanyiwa upasuaji wa jicho lake.
Mwaka 2003 Papa Wemba alifungwa kifungo cha miezi mitatu na nusu jijini Paris kwa tuhuma za kuingiza watu kinyemela nchini humo. Baada ya kutoka jela alikiri kuathirika kisaikolojia na kuamua kuokoka.

October 2003 aliachia albamu yake Somo Trop na kwenye wimbo “Numéro d’écrou”, Papa Wemba anakumbuka jinsi Mungu alivyomtembelea gerezani.
Hadi anafariki, Papa Wemba amesharekodi albamu takriban 43.

KIFO CHAKE

Papa Wemba alifariki Jumapili Alfajiri, April 24 baada ya kuanguka jukwaani alipokuwa akitumbuiza kwenye tamasha la FEMUA mjini Abidjan, Ivory Coast. Video zilizowekwa mtandaoni zinamuonesha akianguka mgongo wakati akiimba.
Alifariki hata kabla kufikishwa hospitali.


Alianguka ghafla

Martin Hubert IKURAMUTSE

Changia hii habari na wenzako.

Comments

Tumia Comments