Burundi yaendelea kukumbwa na machafuko

Ni mwaka mmoja tangu Burundi kuanguka katika ghasia, huku juhudi za amani za kuliondoa taifa hilo la Afrika ya Kati.

Machafuko nchini Burundi yalianza baada ya maandamano makali kufuatia uamuzi wa Rais Pierre Nkurunziza wa kuwania katika uchaguzi wa rais katika muhula mwingine.

Vyama vya upinzani, mashirika ya kiraia pamoja na Kanisa Katoliki vilibaini kwamba Rais Nkurunziza hana haki ya kuania muhula mwengine, kwani atakua amevunja Katiba ya nchi na Mkataba ya Amani na Maridhiano wa Arusha, ambao ni muongozo mama kwa taifa la Burundi.

Hata hivyo, chama cha CNDD-FDD na washirika wake walibaini kwamba Rais Nkurunziza hajavunja Katiba, kwani ana haki ya kugombea muhula mwengine ambao walisema ni wa pili, baada ya kuchaguliwa mara moja pekee na wananchi mwaka 2010.

Maafisa wa ngazi ya juu katika jeshi na polisi wakiongozwa na jenerali Godefroid Niyombare, Mkuu wa zamani wa Majeshi, walijaribu kufanya mapinduzi bila mafanikio, wakati Rais Nkurunziza alikua katika mkutano wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashiriki mjini Dar es Salaam, nchini Tanzania. Ilikua tarehe 13 Mei, 2015 saa saba mchana saa za Afrika ya Kati.

Jenerali Godefroid Niyombare

Baada ya kushindwa kwa jaribio hilo, Mei 14, 2015, serikali ilitangaza marufuku ya maandamano na kuwachukulia watu watakaoingia mitaani kama magaidi. Licha ya tamko hilo la serikali, maandamano yaliendelea na baadaye yaligeuka machafuko, baada ya vikosi vya usalama na ulinzi kujaribu kuzima maandamano hayo kwa kutumia silaha za moto.

Zaidi ya watu 400 wameuawa kwa mujibu wa mashirika ya kimataifa ya haki za binadamu, na watu zaidi ya 200,000 wameyahama makazi yao na kukimbilia nje ya nchi.

Licha ya juhudi za kimataifa za kuliondoa taifa hilo dogo la Afrika ya Kati katika machafuko hayo, bado hali inaendelea kuwa mbaya zaidi huku serikali ikikataa katu kufanya mazungumzo na upinzani, ikidai kwamba baadhi ya vyama vya upinzani viilihusika katika jaribio la mapinduzi.

Martin Hubert IKURAMUTSE

Changia hii habari na wenzako.

Comments

Tumia Comments