Zitto, Lissu wataka Magufuli ataje mshahara, akatwe kodi.

Ikulu yasema wananchi wasubiri utekelezaji wa agizo la vigogo kukatwa mishahara waone ni nani ataguswa, Utumishi wasema utekelezaji umeanza

Rais John Magufuli.
Siku tatu baada ya Rais John Magufuli, kueleza dhamira yake ya kupunguza mishahara ya watumishi wa umma aliosema wanalipwa mpaka Sh. milioni 40 kwa mwezi kwani hataki Tanzania kuwe na mtu analipwa zaidi ya Sh. milioni 15, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu na wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, wametaka kiongozi huyo wa nchi aweke mshahara wake hadharani na ukatwe kodi.

Mwaka 2013, Zitto alisema mshahara wa Rais ambaye kwa wakati huo alikuwa Jakaya Kikwete, ni zaidi ya Sh. milioni 30 na haukatwi kodi.

Kauli ya Magufuli
Akizungumza mkoani Geita Machi 29, mwaka huu, Rais Magufuli alisema : “Nidhamu ya wafanyakazi waliokuwa wamejisahau, walifikiri hapa ni shamba la bibi, nina uhakika tumeanza vizuri, lakini hawajafika idadi ya tunaotaka kuwatumbua...wapo wafanyakazi katika nchi hii wanapata Sh. milioni 40 kwa mwezi na wapo wanaopata Sh. 300,000 kwa mwezi.

Nataka wale wa Sh. milioni 40, na hili nalisema kwa sababu mimi ndiye Rais, tutakata mishahara yao ishuke ili ikiwezekana, wataalam wangu wanafanyia kazi, pasije pakatokea Tanzania, asije akatokea Tanzania mtu anapata mshahara wa zaidi ya Sh. milioni 15.”

Zitto.

Zitto hakuishia hapo, pia alitaja mshahara wa Waziri Mkuu wa wakati huo, Mizengo Pinda, akidai kwamba kwa mwezi analipwa Sh. milioni 26, kati yake kukiwa na Sh. 11.2 za ubunge, Sh. milioni nane za uwaziri na Sh. milioni saba za Waziri Mkuu.

Jana, Zitto alisema azma ya Rais Magufuli ya kutaka kupunguza mishahara ya vigogo wa umma wanaolipwa mpaka Sh. milioni 40, ni njema, lakini ni busara kwanza akaweka wazi mshahara wake na akakubali ukatwe kodi kwa sababu kwa sasa haukatwi.

“Kila mara tumekuwa tukisema ni nini Rais analipwa na wao wanatoka wanasema taarifa tulizotoa siyo sahihi. Ni vyema sasa akaweka wazi mshahara wake na akakubali ukatwe kodi ili iwe mfano kwa watumishi wengine na hata Tanzania iwe mfano wa kuigwa na nchi nyingine,” alisema Zitto.

Lissu
Naye Lissu ambaye pia ni Mwanasheria wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), alisema ni vyema Rais Magufuli na wasaidizi wake wakaweka wazi mishahara yao na siyo ya watumishi wa mashirika pekee.

“Ni vizuri Rais akatuambia mshahara na marupurupu yake yote, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Mawaziri, Manaibu Waziri, Makatibu Wakuu na Manaibu, wasiishie kutaja mishahara ya mashirika pekee,” alisema.

Akitoa maoni kuhusiana na kauli ya Rais, alisema ili apunguze mishahara hiyo, lazima arekebishe sheria inayoruhusu Bodi za Mashirika ya Umma kujipangia viwango vya mishahara kulingana na wanavyozalisha.

Alisema hadi sasa hakuna sheria wala sera inayotaja kiwango halisi cha mshahara bali madaraja kwa watumishi wa Serikali Kuu na serikali za mitaa huku wa mashirika wakiachiwa huru baada ya serikali kuruhusu yajiendeshe kwa faida na kutoa nafasi ya kuwa na miakataba na watumishi na hivyo kuwa na uhuru wa kuamua mshahara.

“Watumishi wa mashirika hayo wanaajiriwa kwa mikataba maalumu ambayo hutaja nafasi anayopewa na kiwango cha mshahara, leo ukipunguza mshahara wake atakwenda mahakamani na kwa ushahidi wa mkataba atashinda kesi,” alisema.

“Rais asifikiri anatawala Tanzania ya Nyerere, bali anatawala Tanzania ya miaka 30 baada ya Nyerere kuondoka. Hana mamlaka ya kupanga mishahara ya watumishi wa mashirika ya umma, kwa kuwa Bodi husika ndiyo zimepewa jukumu hilo. Asizungumze kufurahisha umma kwani atatengeneza vurugu kwenye mashirika husika,” alisisitiza.

Alisema watumishi wa mashirika husika huteuliwa na Rais kwa mujibu wa sheria na Bodi zimepewa mamlaka ya kisheria kupanga mishahara na marupurupu yao bila kuingiliwa, lakini kwa kuangalia uzalishaji uliopo.

Mathalani, alitolea mfano wa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na maji (Ewura), analipwa mshahara mkubwa kuliko Katibu Mkuu wa Wizara ya Niashati na Madini kwa kuwa mmoja umepangwa na Bodi na mwingine kwa mujibu wa Sheria ya Utumishi wa Umma.

CHANZO : NIPASHE

Changia hii habari na wenzako.

Comments

Tumia Comments