Mabalozi wakosoa uchaguzi wa Zanzibar

Tume ya uchaguzi imesema asilimia 67.9 ya wapiga kura walijitokeza
Mabalozi wa nchi za Ulaya na Marekani wamekosoa uchaguzi wa marudio uliofanyika visiwani Zanzibar Jumapili.

Mgombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Dkt Ali Mohammed Shein ametangazwa mshindi wa uchaguzi huo na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).
Chama cha Wananchi (CUF) kilisusia uchaguzi huo.

Mabalozi wa Ubelgiji, Canada, Denmark, Umoja wa Ulaya, Finland, Ufaransa, Ujerumani, Ireland, Italia, Uholanzi, Norway, Uhispania, Sweden, Uswizi, Uingereza na Marekani wamesema uchaguzi huo haukufaa kufanyika bila ya kuwepo kwa maafikiano kuhusu suluhu ya mzozo wa kisiasa visiwani humo.

“Ili uchaguzi uwe wa kuaminika, ni lazima ushirikishe wote na uwe unaakisi nia ya watu,” mabalozi hao wamesema kupitia taarifa.
• Shein atangazwa mshindi wa urais Zanzibar
• Shein azungumza baada ya kupiga kura Zanzibar

“Tunakariri wito wetu kwa Serikali ya Tanzania kutoa uongozi Zanzibar na kufanikisha suluhu kupitia mashauriano kati ya vyama, kwa lengo la kudumisha amani na umoja katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mabalozi hao walionekana kutoa wito kwa Rais John Magufuli kusaidia katika utatuzi wa mzozo huo.
Kiongozi huyo hata hivyo tayari amesema kwamba hataingilia mzozo katika visiwa hivyo.

Dkt Shein baada ya kupiga kura yake Bungi, Unguja
Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa na ZEC, Dkt Shein alipata kura 299,982 ambazo ni sawa na asilimia 91.4 ya kura zilizopigwa.

Mgombea urais wa chama cha ADC Hamad Rashid Mohammed aliibuka wa pili na kura 9,734 (3.0%).
Bw Seif Sharif Hamad wa CUF alipigiwa kura 6,076 (1.9%) licha ya kwamba chama chake kilisusia uchaguzi huo.

Chanzo : BBC

Janvier KARANGWA

Changia hii habari na wenzako.

Comments

Tumia Comments