Mzee Samatta : Nilimzuia Samatta kwenda Yanga


Mzee Samatta

USIKU wa kuamkia Ijumaa ya wiki iliyopita, nahodha mpya wa Taifa Stars na straika wa TP Mazembe, Mbwana Samatta, alifanikiwa kunyakua Tuzo ya Mchezaji Bora wa Afrika wanaocheza ndani baada ya kuwabwaga, Mkongo Robert Kidiaba na Mnalgeria, Baghdad Bounedjah.

Kutokana na mafanikio aliyoyapata straika huyo anayetajwa kujiunga na Genk ya Ubelgiji, Championi lilimsaka baba yake, Ally Samatta kutaka kufahamu maisha ya Mbwana na yaliyojiri baada ya kutangazwa kuwa mshindi.

Unajisikiaje mwanao kuchukua tuzo ?

“Kiukweli najisikia raha sana, namshukuru mwenyezi Mungu kwa sababu furaha niliyokuwa nayo mpaka nililia machozi maana sikutegemea kitu kama hiki kutokea sasa hivi.

Ulishawahi kuhisi kuhusu hilo ?

“Nilishawahi lakini siyo kwa wakati huu kwa sababu alipokuwa ana umri wa miaka saba, kuna kocha mmoja alikuwa anafundisha timu za vijana Simba anaitwa Maka Mwalwisi, aliwahi kunieleza kuwa kijana wangu atafika mbali.
“Unajua alikuwa hakosei kabisa katika kutoa pasi zake kitu ambacho kilimvutia Mwalwisi, naona anafuata nyayo zangu.

Nini kilichobadilika kwa Samatta ?

“Kwanza amekuwa mkubwa na ameongeza umakini uwanjani tofauti na zamani alipokuwa bado kijana, hata hivyo, kuna vitu nilikuwa namuongezea kwa sababu mimi mwenyewe ni kocha, kiukweli vipo vitu vingi nilivyokuwa nampatia kijana wangu kama suala la nidhamu na uvumilivu ndani na nje ya uwanja.

“Kimsingi nilikuwa namjenga katika misingi ya kupambana asiwe mtu wa kukata tamaa au kulalamika uwanjani iwapo inatokea amechezewa vibaya, zaidi nilimtaka kuchukulia ni hali ya kawaida katika mchezo kwa mtu uliyemshinda lazima atakuwa anakuchezea vibaya ili kukudhoofisha,” anasema mzee Samatta.

Kabla ya Samatta kutimikia TP Mazembe akitokea Simba mwaka 2011, aliwahi kucheza na kaka yake, Mohammed Samata katika timu ya Mbagala Market ambayo baadaye ilikuja kuitwa African Lyon, kwa sasa Mohammed anakipiga Mgambo JKT inayoshiriki Ligi Kuu Bara.

Championi lilimuuliza mzee Samatta kwa upande wa Mohammed kama anaweza kufikia mafanikio kama ya mdogo wake ?

“Mmh ! Mohammed, sidhani kama ataweza kufikia huko kwa sababu ana kitu kimoja kinachomponza siku zote licha ya mara nyingi kumuambia, kiukweli anaujua mpira na nimekuwa nikimwambia siku zote kwamba hana nguvu halafu anapenda kucheza soka la Kibrazili.

“Unajua siku zote makocha wanapenda kuwa na mchezaji ambaye akishapunguza watu tayari anaelewa nini cha kufanya, lakini yeye ni tofauti, anapokuwa na mpira ndiyo anazidi kupoa kitu ambacho ni tofauti na Mbwana ambaye akiwa na mpira akili yake inakuwa katika kushambulia tu na hata akikutana na kikwazo atajitahidi ili afikie lengo lake la kwenda kushambulia.

“Lakini Mohammed yeye hapendi kucheza soka la aina hiyo na ndiyo kitu kinachomgharimu lakini kama anashindwa kuelewa ninachomwambia basi hawezi kufanikiwa na kufikia mafanikio ya mdogo wake au zaidi ya hapo, ingawa huwezi jua mipango ya Mungu ipoje.

Unashabikia timu gani hapa nchini ?

“Kwa hapa nyumbani ni shabiki wa Simba, lakini nje ya Tanzania naishabikia Manchester United.

Baba alimgomea kwenda Yanga

“Wakati Mbwana akiwa mdogo, viongozi wa Yanga walinifuata na kutaka kumchukua ili akajiunge na timu yao, lakini niliwakataliwa kutokana na timu hiyo kuwa na historia ya kuwazuia wachezaji kwenda kucheza soka nje ya nchi. Nikaona kama angejiunga nayo basi angeweza kuishia hapahapa tu na kukatisha ndoto zake za kucheza nje.

Vipi kwa upande wa mama Samatta, anapenda soka ?

“Kwa ufupi mke wangu anapenda michezo kwa sababu alipokuwa shule alikuwa akicheza netiboli, halafu mimi nilikuwa namsumbua kila ninapotoka mazoezini aniwekee maji ya moto ya kuoga na hata nilipokuwa nikicheza alikuwa anakuja kuniangalia.

“Tena jambo zuri, amekuwa akimuunga mkono Mbwana.”
Mzee Samatta amefunguka juu ya mtoto wa Mbwana anayeitwa Kareem, alipoulizwa kama anaweza kufuata nyayo za baba yake

“Naamini lazima atafuata nyayo za baba yake kwa sababu wajukuu zangu wote wanacheza mpira na ukizingatia muda wote tunaye hapa kwa kuwa nilimkataza asiende na familia yake DR Congo ili apunguze majukumu na afanye kazi yake vizuri kwani tulimueleza tutamaliza kila kitu kitakachotokea huku,” alisema mzee Samatta ambaye alikuwa polisi enzi zake.

Global Publishers

Changia hii habari na wenzako.

Comments

Tumia Comments