Saudi Arabia yawatimua wanadiplomasia wa Iran

Mfalme wa Saudi Salma bin Abdul-Aziz al-Saud.

Saudi Arabia imevunja uhusiano wa kidiplomasia na Iran, baada ya waandamanaji kuuvamia ubalozi wake mjini Tehran na kuuchoma moto, na kutoa saa 48 kwa wanadiplomasia wa Iran kuondoa nchini humo.

Hatua ya Saudi Arabia ilikuja saa chache baada ya waandamanaji kuuvamia na kuuchoma moto ubalozi wake mjini Tehran, katika kupinga mauaji ya kiongozi wa Kishia Sheikh Nimr al-Nimr.

Mauaji ya Nimr pamoja na wengine 46 - ambayo ndiyo makubwa zaidi kufanywa kwa wakati mmoja katika kipindi cha miongo mitatu na nusu - yamebainisha wazi migawanyiko mikubwa inayoikabili kanda ya Mashariki ya Kati, ambako waandamanaji waliingia mitaani kuanzia Bahrain hadi Pakistan kuyapinga.
Al-Nimr alikuwa mtu muhimu katika maandamano ya Washia wachache wa Saudi Arabia, yaliyohamasishwa na uasi wa umma katika mataifa kadhaa ya Kiarabu, hadi alipokamatwa mwaka 2012.

Alitiwa hatiani kwa makosa ya ugaidi, lakini alikanusha kuchochea vurugu. Kiongozi wa juu kabisa nchini Iran, Ayatollah Ali Khomenei, alisema Saudi Arabia italipa gharama kubwa kwa mauaji ya Nimr.

Waziri al-Jubeir alisema mashambulizi dhidi ya balozi zake nchini Iran ni mwendelezo wa sera za kibabe za utawala wa Tehran katika kanda hiyo, zinazolenga kuvuruga usalama na kueneza ugomvi na vita, ambavyo amesema vinathibitishwa na hatua ya Iran kuwapa hifadhi viongozi wa Al-Qaeda tangu mwaka 2011, na pia kuwapatia ulinzi baadhi ya walioshiriki katika uripuaji wa majengo ya al-Khobar mwaka 1996.

"Kwa kuzingatia ukweli huu, Saudi Arabia inatangaza kuvunja uhusiano wa kidiplomasia na Iran, na inaomba kwamba wanadiplomasia wote walioko ubalozini, ubalozi mdogo na ofisi tanzu zote kuondoka katika muda wa saa 48," alisema Al-Jubeir.

Iran ilisema iliwakamata watu 44 kuhusiana na mashambulizi ya ubalozi, na rais Hassan Rouhani akawaelezea waandamanaji hao kuwa wenye itikadi kali, na kwamba mashambulizi dhidi ya balozi za Saudi hayakuwa na uhalali wowote.
Visasi vyaanza

Nchini Iraq, misikiti miwili ya Kisunni imeripotiwa kushambuliwa kwa mabomu katika mkoa wa katikati mwa nchi hiyo wa Hilla, huku muadhini akiuawa kwa kupigwa risasi karibu na nyumbani kwake mjini Iskandariya, kulingana na maafisa wa polisi na wahudumu wa afya.

DW

Changia hii habari na wenzako.

Comments

Tumia Comments