Azam FC yapania kuishusha Yanga

Kocha wa Azam Stewart Hall.

Wakati Kocha wa Mtibwa Sugar, Mecky Mexime akitamba kuitumia mechi yao ya leo dhidi ya Azam FC kulipa kisasi cha kufungwa magoli 5-2 msimu uliopita, wapinzani wao hao wameapa ’kufia’ uwanjani kuhakikisha wanashinda na kuing’oa Yanga kileleni.

Mtibwa, mabingwa mara mbili wa Tanzania Bara 1999 na 2000, walikumbana na kipigo hicho kikubwa msimu uliopita wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) kwenye Uwanja wa Azam jijini Dar es Salaam Februari 11 mwaka huu kabla ya kutoka sare ya bao 1-1 kwenye Uwanja wa Manungu katika mechi yao ya pili msimu uliopita.

Mexime alisema anatambua Azam ni timu kubwa kwa sasa na kutokana na hilo, wamejiandaa vizuri kuhakikisha wanashinda mechi hiyo kabla ya kuikabili tena klabu hiyo katika mechi yao ya kwanza ya Kundi B la Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar Januari 2 mwakani.

"Ndiyo, tulifungwa 5-2, lakini hizo ni rekodi ambazo tunaweza kuzifuta. Mechi itakuwa ngumu, tumejipanga vizuri msimu huu, ninaamini tutafanya vizuri katika mechi hiyo," alisema nahodha huyo wa zamani wa Mtibwa na Taifa Stars.

Kwa upande wake, kocha wa mabingwa wapya wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC (Hall) alisema jana kuwa ushindi katika mech ya leo "ni lazima" ili kurejea kileleni mwa msimamo wa VPL kabla ya mwaka kumalizika.

Azam inayoshika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ikiwa na mtaji wa pointi 32, itakwaruzana na Mtibwa katika mchezo huo wa kiporo wa raundi ya sita uliopigwa kalenda kupisha mechi ya Taifa Stars dhidi ya Malawi. Ushindi wowote utawafanya Wanalambalamba kufikisha pointi 35 na kuiteremsha Yanga iliyojikusanya pointi 33.

Hall alikaririwa na mtandao rasmi wa Azam FC jana akieleza kuwa mipango yao ni kushinda mchezo huo, huku akikiri kuwa utakuwa mgumu kutokana na ubora wa kikosi cha Mexime kinachokamata nafasi ya tatu kwa sasa.

“Tumejipanga kushinda na lazima tufanye hivyo, tunataka kurejea namba moja kwenye msimamo, ninajua mchezo utakuwa mgumu kama ulivyokuwa kwa Kagera Sugar, lakini tumejipanga kwa changamoto zozote uwanjani,” alisema.

Hall aliongeza kuwa atawakosa wachezaji wanne kutokana na majeraha ; mabeki Aggrey Morris na Erasto Nyoni aliyeumia nyama za juu ya paja katika mchezo dhidi ya Kagera Sugar, mshambuliaji Ame Ally Amour na beki David Mwantika aliyefiwa na mdogo wake mwishoni mwa wiki iliyopita.

KOMBE LA MAPINDUZI

Katika hatua nyingine, Hall amefurahishwa na ratiba ya Kombe la Mapinduzi iliyotolewa juzi, akieleza kuwa amepanga kuitumia michuano hiyo kuwapa kipaumbele cha kucheza wachezaji ambao hawapata nafasi kubwa ya kucheza VPL msimu huu.

Azam imepangwa Kundi B kwenye michuano hiyo pamoja na Yanga, Mtibwa Sugar na Mafunzo ya Zanzibar,
Matajiri hao wa Tanzania, watafungua dimba kwa kucheza na Mtibwa Sugar Jumapili saa 2:15 usiku, itacheza na Yanga Jumanne saa 2:15 usiku kabla ya kumaliza mchezo wa mwisho wa makundi kwa kuchuana na Mafunzo Januari 7.
Vinara wawili wa kundi hilo na la lile la A lenye timu za Simba, Jamhuri, JKU na URA, watafuzu kwa hatua ya nusu fainali itakayochezwa kwa siku mbili Januari 9 na 10 (zote saa 2.15 usiku), huku mchezo wa fainali ukipigwa Januari 13.

“Ratiba iko vizuri, tunatakiwa kucheza na Mtibwa Sugar, Yanga na Mafunzo, kwetu ni jambo jema, tutaitumia michuano ya Mapinduzi kuwapa kipaumbele wachezaji ambao hawajacheza msimu huu, ninataka kuona uwezo wa kina Ame Ally, Allan Wanga, Messi (Ramadhan Singano), Gardiel Michael, Vialli (Khamis Mcha), Mudathir (Yahya), pia David Mwantika.

Msimu huu Azam imepania kubeba vikombe kwenye michuano yote inayoshiriki kuanzia VPL, Kombe la FA na Kombe la Mapinduzi, huku ikipanga kutinga hatua ya robo-fainali ya Kombe la Shirikisho barani Afrika mwakani.

IPPmedia

Changia hii habari na wenzako.

Comments

Tumia Comments