Alshabaab waua polisi 2 Kenya

Maafisa wawili wa polisi wameuawa katika shambulizi la wapiganaji kutoka kundi la Kiislamu al-Shabab kutoka Somalia.

Shambulizi hilo lilitokea katika mji wa El Wak ambao uko katika eneo la mpaka kati ya Kaskazini Mashariki mwa Kenya na Somalia.

Polisi hao wanaaminika kuwa ndani ya gari lao wakishika doria katika barabara moja kabla yao kushambuliwa ghafla na wapiganaji hao

Wawili kati yao walipoteza maisha yao huku wengine wawili wakijeruhiwa vibaya.
Shambulizi hili la leo limetokea takriban kilomita 5 pekee kutoka pahala ilikoshambulia basi ya usafiri wa umma mapema wiki iliyopita na kuua watu wawili.

Vyanzo vya wapiganaji hao wa Al-Shabab pia vinadai kuwa walitekwa gari la kijeshi.
Dai hilo halijathibitishwa.

Hapo jana mtu anayeshukiwa kuwa mpiganaji wa Al Shabaab aliuawa alipokuwa akitega bomu la ardhini katika barabara hiyo ya Lafey – El Wak.

Kumekuwa na mashambulizi kadhaa katika kanda hiyo katika wiki za hivi karibuni.
Kundi hilo linadaiwa kuwa limegawanyika kuwa mawili baada ya baadhi yao kukubali kuungana na wanamgambo wa Islamic State.

Kundi hilo lililojitenga linadaiwa kuongozwa na Gamadhere aka Kuno wanaiunga mkono ISIS.

Mashambulizi haya yaliyochacha kwa mjibu wa Inspekta mkuu wa polisi nchini Kenya Joseph Boinett yanalenga kuwaonesha wadhamini wao kuwa wana uwezo wa kufanya mashambulizi ndani ya Kenya.

Kenya ilituma askari wake nchini Somalia mwaka 2011 ili kujaribu kushinda wapiganaji hao wa Kiislamu na kuisaidia serikali dhaifu.

BBC

Changia hii habari na wenzako.

Comments

Tumia Comments