MATATIZO YA UPEVUSHAJI MAYAI

Tatizo hili kitaalamu linaitwa ‘Ovulatory Factor’, husababishwa na kasoro mbalimbali kwenye mfumo wa homoni ambao hutokana na uwepo wa uvimbe katika ubongo

Kulingana na Global Publishers Katika mfumo wa homoni, uvimbe wa vifuko vya mayai, vifuko vya mayai kushindwa kuzalisha vichocheo au mayai yenyewe, kuchelewa kwa mwili wa mwanamke kupevuka, magonjwa mbalimbali kama ya ini, figo, tezi shingoni au goita na unene kupita kiasi.

Matatizo haya huambatana na dalili mbalimbali kutegemea na jinsi tatizo linavyotokea, mfano kutokuota vinyweleo sehemu za siri na kwapani, kutokuota matiti au kuchelewa kupata mabadiliko hayo. Kuota ndevu na vinyweleo mikononi na miguuni, hata tumboni na kifuani kwa wanawake. Kutokupata damu ya hedhi kabisa au kufunga kupata kwa muda mrefu.

Matiti kutoa majimaji au maziwa, kupoteza hisia na raha ya tendo la kujamiiana. Kwa hiyo mwanamke anaweza kuwa na zote au mojawapo ya dalili hizo kutegemea na athari zilizojitokeza kwake.

MATATIZO KATIKA NYONGA

Ni mojawapo ya matatizo makubwa yanayoathiri uzazi kwa mwanamke. Matatizo katika nyonga yaani chini ya tumbo, toka katika usawa wa kitovu hadi ukeni.

Mwanamke anaweza kupata maambukizi mbalimbali, mfano ugonjwa wa kidole tumbo ambao wengi wamezoea kuita “Apendix’ lakini kitaalamu unaitwa ‘Appendicitis’,

aambukizi sugu katika viungo vya uzazi au ‘PID’, kushikamana kwa kizazi kutokana na makovu yanayosababishwa na kusafisha kizazi mara kwa mara, aidha baada ya mimba kuharibika au kudhani kwamba ni msaada wa kuharakisha kupata mimba, kasoro katika tabaka la ndani la kizazi kuwa nje ya kizazi, pia huchangia kwa kiasi kikubwa ugumba.

Matatizo mengine yanayoweza kusababisha ugumba ni uvimbe wa ‘fibroid’, inategemea na sehemu ulipo, kasoro za kuzaliwa nazo za viungo vya uzazi.

Dalili kuu za matatizo haya ni maumivu sugu chini ya tumbo, kuvuruga mzunguko wa hedhi au kutokupata hedhi, maumivu wakati wa tendo la kujamiiana, kutokwa na uchafu ukeni kwa muda mrefu wenye muwasho na harufu.

MATATIZO KATIKA SHINGO YA KIZAZI

Tatizo hili linaweza kuwa la kuzaliwa nalo, likasababishwa na matumizi ya baadhi ya madawa kwa mama mjamzito ukajikuta unazaa mtoto anapata kasoro katika viungo vyake mojawapo ni viungo vya uzazi.
Tatizo katika viungo vya uzazi pia linaweza kusababishwa na maambukizi, upasuaji au magonjwa sugu katika uke au shingo ya uzazi.

Mwanamke mwenye tatizo hili hulalamika maumivu wakati wa tendo la kujamiana au kutokwa na damu ukeni wakati wa tendo.

Vile vile kutokwa na uchafu ukeni unaotoa harufu au muwasho, ingawa wakati mwingine anaweza kupata ute mzito daima.

VIGEZO VYA UCHUNGUZI

Katika suala zima la ugumba kwa mwanaume na mwanamke lazima kuwepo na vigezo vya uchunguzi. Kwa mwanamke mambo ya kuangalia ni historia yake katika matumizi ya madawa ya tiba alipokuwa mdogo au hata kama mama yake aliwahi kutumia aina fulani za madawa wakati wa ujauzito.

Tutaangalia kama ulivunja ungo kwa wakati muafaka, mfano uliwahi sana au ulichelewa sana. Muda muafaka ni kati ya miaka 12 hadi 16. Kufahamu mzunguko wako wa hedhi unavyoenda na kiwango cha damu unachopata, kama ulishawahi kutumia njia za kisasa za uzazi wa mpango, Je, ulishawahi kupata mimba ? Na ulizaa au iliharibika ?

Vile vile inahitajika kujua kama ulishawahi kufanyiwa upasuaji wowote chini ya tumbo mfano kutoa uvimbe, mimba nje ya kizazi, kuzaa mtoto kwa upasuaji.

Ni muhimu pia daktari akafahamu endapo ulishawahi kupata maambukizi yoyote katika viungo vya uzazi, madawa uliyokwishawahi kutumia kwa muda mrefu, ulaji wako wa vyakula, kama unakunywa pombe au unavuta sigara.
Kwa upande wa mwanamke, vigezo ni kama una kasoro katika viungo vyako vya uzazi, mfano uume ni mfupi sana, tundu la mkojo limekaa upande, kasoro katika korodani au kende kama zipo, zimevimba, zimesinyaa au ndogo sana, hazipo au ipo moja, zinauma au moja ndogo na nyingine kubwa.

Pia utahitajika kujua kama ulishawahi kusumbuliwa na maambukizi katika njia ya mkojo kwa muda mrefu, mfano kisonono au yutiai za mara kwa mara, maumivu wakati wa kukojoa au kutokwa na majimaji au manii katika njia ya mkojo.

Inahitajika kujua historia yako kama ulishawahi kumpa mimba mwanamke, kama una mtoto. Ufanyaji wako wa tendo la kujamiiana pia daktari itabidi ajue endapo huwezi kabisa, kumudu, unawahi kumaliza, unachoka sana baada ya tendo au unashindwa kurudia, au uume hauna nguvu za kutosha.

Ni muhimu kuelezea kama unakunywa pombe, unavuta sigara au unatumia madawa ya kulevya kama bangi, mirungi na mengineyo. Vyote hivi huathiri uzazi kwa kiasi kikubwa. Je ulishawahi kufanyiwa upasuaji hasa wa henia au ngiri ya kushuka, busha, vyote inabidi vijulikane.

Matumizi ya madawa ya kulevya ya hospitali kwa muda mrefu, mfano dawa kwa ajili ya vidonda vya tumbo, kifafa, moyo, kifua kikuu na mengineyo. Ulaji wako wa chakula na ufanyaji mazoezi, vile vile kuangalia unanyoa sehemu za siri na makwapani baada ya muda gani, kwani nayo huchangia kuashiria baadhi ya dalili.

Kwa hiyo, ukiangalia kwa undani kuhusiana na suala zima la kutopata mtoto, siyo tu kwamba mtu anatumia dawa fulani na kufanikiwa.

Pia suala hili halitibiwi kwa hisia na utabiri, bali ni suala la kisayansi na linahitaji uchunguzi wa kina na tiba za hospitali.

Vyanzo vya matatizo haya ni vingi na tofauti ni kubwa inayomtokea kila mwenye tatizo. Tumeona vigezo.
NINI CHA KUFANYA ?

Katika makala ijayo tutaona kwa undani kuhusiana na vipimo vya msingi, tiba na ushauri ili usije ukapata tatizo au kama ulikuwa nalo likatibika, basi lisijirudie.

Tatizo hili la kutokupata mtoto au ugumba kama tulivyokwishaona hapo awali, linawahusu mke na mume, yaani watu wawili wanaotafuta mtoto kwa mwaka mzima lakini aidha mimba zinatoka au hafanikiwi kabisa. Pia tunasema tendo hilo la kujamiiana linafanyika kikamilifu.

Kufanya kikamilifu maana yake uume unaingia ukeni na tendo hilo linafanyika zile siku za kupata ujauzito. Lini mwanamke anapata ujauzito ? Au siku za hatari za kupata ujauzito ni zipi ? Kaa sawa kwa kuendelea kusoma makala hizi tutaelezea kwa undani.

Kwa hiyo, kama tulivyoelezea, hakuna sehemu ambapo utapata tiba sahihi ya matatizo haya ya kutopata ujauzito zaidi ya kwenda katika Hospitali za mikoa ambapo utakutana na madaktari bingwa wa matatizo ya uzazi, utafanyiwa vipimo vya kisayansi wewe na mwenzio na kupata tiba sahihi kufuatana na jinsi tulivyoyachambua hayo matatizo.

Global Publishers

Changia hii habari na wenzako.

Comments

Tumia Comments