Niyonzima asimamishwa Yanga, akatwa mshahara

Haruna Niyonzima

KIUNGO wa Yanga SC, Haruna Hakizimana Fadhil Niyonzima atapokea nusu mshahara kwa muda usiojulikana, baada ya kusimamishwa na uongozi wa klabu hiyo kwa utovu wa nidhamu.

Katibu Mkuu wa Yanga SC, Dk. Jonas Tiboroha amesema kwamba, klabu imemsimamisha Niyonzima kwa muda usiojulikana baada ya kurudia kuchelewa kujiunga timu kufuatia ruhusa maalum.

Dk Tiboroha amesema uamuzi huo umefikiwa na kikao cha Kamati ya Mashindano, chini ya Mwenyekiti wake, Isaac Chanji jana mjini Dar es Salaam.
“Amekuwa akifanya mambo ambayo yanaonyesha wazi ni ukiukaji mkataba hasa katika masuala ya utendaji.

“Lakini amekuwa akionyesha utovu wa nidhamu. Kwani licha ya kukaa naye pamoja na kuzungumza naye kuhusiana na hali hiyo bado amerudia.
“Tulikaa naye Novemba 4, ilikuwa pale Protea Hotel. Tukajadiliana na mwisho akaomba msamaha na kuahidi asingerudia tabia hiyo ya kuwa mchelewaji kurejea kazini kila anapokwenda Rwanda.

“Lakini amerudia safari hii, tena akijua wazi alijiunga na timu ya taifa ya Rwanda bila taarifa kwa klabu.

Halafu baada ya fainali ya Cecafa akazima simu kabisa,” alisema Dk Tiboroha.
Maamuzi hayo yamefikiwa kufuatia Niyonzima kushindwa kujirekebisha licha ya kuonywa mara kadhaa juu ya desturi hiyo isiyopendeza.

Niyonzima aliibuka mapema wiki hii mjini Dar es Salaam na kujisalimisha klabuni akiwa amefungwa plasta gumu (PoP), maarufu kama ‘hogo’, baada ya Yanga SC kusema itamchukulia hatua za kinidhamu kwa kitendo cha kuchelewa kurejea katika timu.

Nahodha huyo wa Rwanda aliruhusiwa kwenda kuichezea timu yake ya taifa katika Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge nchini Ethiopia, lakini baada ya mashindano akachelewa kurejea Dar es Salaam.

Global Publishers

Changia hii habari na wenzako.

Comments

Tumia Comments