UNSC yataka kuimarisha uwepo wa Umoja wa Mataifa Burundi

Katika mji wa New York, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepitisha Alhamisi wiki hii azimio kuhusu Burundi. Ufaransa iliwasilisha rasimu hiyo, inayotishia kuwachukulia vikwazo wahusika wa machafuko. Hatimaye, azimio hilo limepasishwa.

Azimio hili lilikua katika majadiliano tangu Jumatatu iliyopita kwa ombi la Ufaransa ambayo inaendelea kutiwa wasiwasi kuhusu hali inayoendelea kushuhudiwa Burundi na hatari ya mauaji ya halaiki ambayo yanaweza kutokea wakati wowote, kama hayatazuilia haraka. Azimio hilo limepitishwa bila kupingwa na wajumbe kumi na tano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Balozi wa Ufaransa katika Umoja wa Mataifa, François Delattre, amesema ni hatua muhimu iliopigwa katika matumaini ya kuona mazungumzo ya kitaifa yatakayowashirikisha wadau wote nchini Burundi yanaanzishwa.

Azimio hili linatoa wito hasa kwa mazungumzo ya haraka kati ya serikali na upinzani. Lakini ni azimio lenye tafauti kidogo na nakala iliyosambazwa wiki hii. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeamua kuweka mbele Umoja wa Afrika (AU) katika utatuzi wa mgogoro wa Burundi. Na hiyo ndio njia pekee iliokubaliwana wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutoka Afrika , huku Urusi na China wakichukulia hali hiyo kama mgogoro wa ndani.

Vikwazo

Azimio hili linataja uwezekano wa vikwazo kwa kuzingatia tangazo la Umoja wa Afrika la Oktoba 17. Tangazo ambalo lilitaja uwezekano wa vikwazo kwa wahusika wa machafuko Burundi kama vile marufuko ya kusafiri na kuzuia mali ya wahusika wa machafuko.

Kutumwa kwa vikosi vya Umoja wa Mataifa

Azimio hilo halikutaja wazi kupelekwa kwa vikosi vya Umoja wa Mataifa nchini Burundi. Azimio hilo linamuomba Ban Ki-moon, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kutuma timu ya ya Umoja wa Mataifa nchini Burundi ili kuhakikisha upatanishi wa kisiasa. Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa pia ameteuliwa nchini humo. Ni Jamal Benomar ambaye alikuwa mjumbe maalum wa zamani nchini Yemen.

Kuhusu askari wa kulinda amani au kikosi cha polisi, azimio hili linamuomba Katibu mku wa Umoja wa Mataifa kuwa tayari katika kutuma kikosi cha wanajeshi wa Umoja wa mataifa nchini Burund iwap hali ya usalama itaendelea kuzorota. Lakini Idara ya Oparesheni za Kulinda Amani mjini New York, ni imesema yote yanawezekana, ikiwa ni pamoja na kutuma kikosi cha Umoja wa Mataifa kilioko nchi jirani ya Congo. Taarifa ambayo imethibitishwa baada ya mkutano huo wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Balozi wa Uingereza.

RFI Kiswahili

Changia hii habari na wenzako.

Comments

Tumia Comments