UNSC inakutana leo kujadili hali ya Burundi

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kwa ombi la Ufaransa, linakutana leo Jumatatu Novemba 9, kujadili hali mbaya inayoendelea kushuhudiwa nchini Burundi.

Juma lililopita Ssirika la kimataifa linalohusika na kutatua migogoro kwa njia ya amani, International Crisis Group (ICG), lilisema kuwa hali ya Burundi inatisha, na lilielezea wasiwasi wake kuhusu kauli ziliyotolewa hivi karibuni na viongozi wa nchi hiyo ikiwa ni pamoja na Rais Pierre Nkurunziza, na viongozi wengine dhidi ya wakazi wa maeneo ambayo ni kitovu cha maandamano dhidi ya muhula wa tatu wa rais wa nchi hiyo.

Internatinal Crisis Group ilizifananisha kauli hizo na zile ziliyotolewa miaka ya 1990 na viongozi wa zamani wa Rwanda kabla ya mauaji ya kimbari ya mwaka 1994. Shirika hilo limeendelea kubaini kwamba bila shaka viongozi wa Burundi wamedhamiria mpango wa kuwaangamiza raia wote wanaopinga muhula wa tatu wa Rais Nkurunziza.

Hayo yanajiri wakati raia wa baadhi ya maeneo ambayo ni kitovu cha maandamano dhidi ya muhula wa tatu wa Rais Pierre Nkurunziza, hususan Mutakura, Cibitoke na Musaga waliyahama makazi yao na kukimbilia katika maeneo jirani na mikoani, kufuatia kutamatika Jumamosi usiku kwa muda uliyotolewa na viongozi wa Burundi wakiwataka raia wa maeneo hayo wanaomiliki silaha kujisalimisha, la sivyo watakiona cha mtimakuni.

Mashirika ya kimataifa ya haki za binadamu na yale yanayoendesha shughuli zao nchini Burundi yamekua yakivishooshea kidole vikosi vya usalama kuhusika katika visa mbalimbali vya mauaji na ukiukwaji wa haki za binadamu.

Hali hii inayojiri nchini Burundi imesababisha watu zaidi ya 200,000 kuyahama makazi yao na kukimbilia nchi jirani. Kwa mujibu wa mashirika yanayotetea haki za binadamu zaidi ya watu 200 wameuawa katika vurugu zinazoendelea nchini Burundi, wengi wao wameuawa na vikosi vya usalama, kwa mujibu wa mashirika hayo.

Hata hivyo serikali ya Burundi imeendelea kuyanyooshea kidole cha lawama baadhi ya mataifa ya magharibi na taasisi za kimataifa, hususan Ubelgiji, Marekani, Umoja wa Ulaya na Umoja wa Afrika, kuwasaidia wapinzani kwa kuendelea kuhatarisha usalama wa taifa hilo.

RFI Kiswahili

Changia hii habari na wenzako.

Comments

Tumia Comments