Magufuli afanya ziara ya kushtukiza Hazina Kuu

Rais mpya wa Tanzania John Magufuli leo amefanya ziara ya kushtukiza katika Hazina Kuu siku moja tu baada yake kuapishwa.

Rais huyo amefanya ziara hiyo fupi kutoka ikulu muda mfupi baada ya kumuapisha Mwanasheria Mkuu George Mcheche Masaju.

Bw Masaju aliteuliwa mara ya kwanza kuwa Mwanasheria Mkuu na Rais Mstaafu Jakaya Kikwete Januari mwaka huu baada ya kujiuzulu kwa George Werema.

Bw Masaju alikuwa ameteuliwa kuwa mwanasheria mkuu Januari na Rais Kikwete ambaye sasa amestaafu

Bw Magufuli hakuzungumza rasmi na wanahabari baada ya kumaliza ziara hiyo.
Hata hivyo, mwandishi wa BBC Tulanana Bohela anasema kuna uwezekano amezungumza na maafisa wa hazina kuu kuhusu hali ya mikopo ya wanafunzi.
Wakati wa kampeni, Bw Magufuli aliahidi kufanya elimu kuwa bila malipo kuanzia shule za msingi hadi shule za sekondari.

Taarifa kutoka ikulu ya Dar es Salaam zinasema kwenye mkutano na maafisa wakuu wa Wizara ya Fedha, Bw Magufuli aliwaagiza kuziba mianya yote inayotumiwa na wakwepa kodi.

Bw Magufuli ameagiza Bunge lifunguliwe Novemba 17 na anatarajia kuwasilisha jina la Waziri Mkuu wake kwa bunge hilo Novemba 19.

BBC Kiswahili

Changia hii habari na wenzako.

Comments

Tumia Comments