Rais wa Misri atetea sheria kali za usalama

Rais wa Misri Abdul Fattah al-Sisi ametetea sheria kali za kiusalama zilizopitishwa na serikali yake na kusema taifa lake bado linadumisha demokrasia.

Akizungumza na BBC kabla ya ziara yake Uingereza, Bw Sisi amesema Misri inatishiwa na makundi ya kigaidi na ana wasiwasi kwamba hatua zisipochukuliwa huenda likaathirika kama mataifa mengine jirani.

Alisema hali nchini Misri ni tofauti na hali Ulaya.

Bw Sisi alikuwa kiongozi wa jeshi na aliongoza mapinduzi dhidi ya Rais Mohammed Morsi mwaka 2013 baada ya maandamano ya raia.

Tangu wakati huo, mamia ya watu wameuawa na wengine zaidi ya 40,000 wanaaminika kufungwa jela kwenye operesheni kali ya kukabiliana na wapinzani wa serikali.

Wengi ni wafuasi wa chama cha Bw Morsi, Muslim Brotherhood, ambacho kilipigwa marufuku. Wengine ni wanaharakati wanaodaiwa kuvunja sheria ya kupinga maandamano mwaka 2013. Sheria hiyo inaipa wizara ya masuala ya ndani mamlaka ya kupiga marufuku mkusanyiko wowote wa watu zaidi ya 10.

Akizungumza katika mahojiano na BBC mjini Cairo kabla ya ziara yake ya kwanza rasmi Uingereza, Bw Sisi alisema Misri bado inapiga hatua katika kufikia demokrasia, safari iliyoanza baada ya kuondolewa madarakani kwa Rais Hosni Mubarak kufuatia maandamano 2011, lakini inahitaji muda.

"Tunataka kutekeleza mapenzi ya watu wa Misri,” alisema.

“Wamekuwa wakiitisha mabadiliko haya kwa miaka minne. Tunataka kutimiza maombi yao na tutajaribu kadiri ya uwezo wetu kuwapa demokrasia ya kufana siku za usoni.”

Bw Sisi kadhalika alisema kukosa kujitokeza kwa wingi kwa watu kushiriki uchaguzi wa ubunge mwezi jana si jambo ambalo halikutarajiwa, lakini pia akasisitiza kwamba si ishara ya watu kutoridhishwa na utawala wake.

Aidha, alitetea sheria ya kukabiliana na ugaidi zilizopitishwa Agosti, ambazo wanaharakati wanasema zinakiuka haki za kibinadamu.

"Ni vyema kuangalia haki za kibinadamu Misri. Lakini kwa mamilioni ya watu wanaokabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi, si ingekuwa bora kuwaangalia pia ?”


BBC Kiswahili

Changia hii habari na wenzako.

Comments

Tumia Comments