Mihuri yatia doa upigaji kura

Mgombea urais wa chama cha TLP, Macmillan Lyimo (kushoto) akipewa maelekezo na Aliko Mkumbwa ambaye ni Msimamizi wa uchaguzi katika kituo cha kupigia kura Kata ya Njia Panda, Vunjo, namna ya kujaza fomu maalumu ili aweze kupiga kura kituoni hapo kutokana na kutojiandikisha kituoni hapo, mkoani Kilimanjaro jana.

Picha na Dionis Nyato

Kwa ufupi

Changamoto hiyo ya wino ilijitokeza pia katika baadhi ya maeneo jijini Dar es Salaam, hali iliyosababisha upigaji kura kusimama kwa saa kadhaa.

Dar/Mikoani. Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imelazimika kutumia mihuri ya mwaka 2010 katika vituo mbalimbali vya Jimbo la Morogoro Mjini baada ya mihuri ya mwaka huu kuwa na matatizo.
Changamoto hiyo ya wino ilijitokeza pia katika baadhi ya maeneo jijini Dar es Salaam, hali iliyosababisha upigaji kura kusimama kwa saa kadhaa.

Akizungumzia dosari hiyo, msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo, Teresia Mahongo alisema hali hiyo ilianza kujitokeza mapema asubuhi katika baadhi ya vituo.

Mahongo alisema baada ya kujitokeza dosari hiyo, aliwasiliana na NEC pamoja na viongozi wa vyama vya siasa na kukubaliana kwa pamoja kutumia mihuri ya mwaka 2010.
“Tume ilitoa ruhusa ya kutumia mihuri ya mwaka 2010 ili kuhalalisha kura zitakazopigwa kwa sababu bila ya kugongwa muhuri kura haiwezi kuwa halali, na hatua hiyo imeafikiwa na viongozi wa vyama vyote vya siasa ambavyo vinashiriki uchaguzi,” alisema Mahongo.

Aliwataka wananchi pamoja na vyama vyote vya siasa kuiamini mihuri hiyo kwa kuwa isingewezekana kusitisha uchaguzi kwa sababu ya kuharibika kwa mihuri.

Awali, mgombea ubunge kwa tiketi ya Chadema, Marcus Albanie hakukubaliana na uamuzi wa kutumia mihuri hiyo, akituhumu kuwapo njama za kuvuruga uchaguzi.
“Kama mihuri hiyo haikuwa na ubora unaokubalika, kwa nini waliisambaza kwenye vituo” Na je itaaminika vipi wakati mihuri hiyo ilishatumika katika uchaguzi uliopita ?” alihoji Albanie.

Lakini baadaye jioni jana alisema amekubaliana na uamuzi huo baada ya kueleweshwa mazingira yaliyosababisha kufikiwa kwa uamuzi wa kutumia mihuri ya mwaka 2010.

Kwa upande wake, msimamizi msaidizi wa kituo cha kupigia kura cha Kata ya Mtoni ambacho ni miongoni mwa vituo vilivyokuwa na dosari hiyo, Patrokil Silayo alisema mihuri iliyoletwa mwaka huu haina ubora kwa kuwa inavunjika na mingine kushindwa kutoa wino.

Hata hivyo, alisema uchaguzi unaendelea kwa kutumia mihuri ya mwaka 2010 baada ya kupewa ruhusa na msimamizi wa uchaguzi wa jimbo.

Dosari hiyo pia ilionekana katika vituo mbalimbali vilivyopo Jimbo la Morogoro Kusini na Morogoro Kusini Mashariki

Mbagala

Wakati hayo yakiendelea Morogoro, wakazi wa kitongoji cha Jeshi la Wokovu, Mbagala Kuu walichelewa kuanza kupiga kura kutokana na ukosefu wa mihuri na wino.
Gazeti la Mwananchi lilishuhudia idadi kubwa ya watu wakiwa katika kituo hicho wakijadili masuala mbalimbali ya uchaguzi.
“Tupo hapa nje kwa muda mrefu, lakini hatujajua hatima yetu kama tutapiga kura au la. Vituo vimefunguliwa saa 3:00 asubuhi, lakini hakukuwa na vifaa hivyo zoezi lilisimama kwa muda,” alisema Ally Mlapakolo mkazi wa Mbagala Kuu.

Msimamizi wa kituo hicho, Yahya Yusuf Msham alikiri kuwapo kwa tatizo hilo. “Ni kweli kabisa kulikuwa na matatizo, lakini kwa sasa tumeweka mambo sawa. Tumeazima muhuri na wino kutoka kituo cha jirani,” alisema.

Viongozi wa NEC wa Jimbo la Temeke waliliambia Mwananchi kuwa upungufu wote unafanyiwa kazi.

“Tumepata taarifa ya kukosekana kwa baadhi ya vifaa, tunalifanyia kazi suala hilo ili kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa,” alisema Lusa Edwin msimamizi msaidizi wa uchaguzi, Jimbo la Mbagala.
Hadi Mwananchi inaondoka kwenye kituo hicho bado kasi ya uandikishaji ilikuwa ndogo ukilinganisha na wingi wa idadi ya watu.

Kinondoni

Katika baadhi ya vituo vya Jimbo la Kinondoni- kituo cha Kijitonyama C1 na C2- kulikuwa na uhaba wa mihuri jambo lililosababisha upigaji kura kusuasua.
Tabata

Kama ilivyokuwa katika maeneo mengine, wapigakura wa Tabata Kimanga walijikuta wakisubiri kwa muda mrefu kutimiza azma yao kutokana na kukosekana kwa mihuri.

Mmoja wa wakazi wa kituo cha Kimanga Darajani, Juma Mzindakaya alisema tatizo la mihuri linaonekana kuwa kubwa na linazorotesha kazi hiyo.

Mwananchi

Changia hii habari na wenzako.

Comments

Tumia Comments