Martial asaidia Man Utd kuondoka na sare Urusi

Anthony Martial aliisaidia Manchester United kunusuru alama moja wakicheza dhidi ya CSKA Moscow katika Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya baada yake kusababisha penalti.

Bao la Martial dakika ya 65 liliwawewezesha miamba hao wa Uingereza kuondoka Urusi na sare ya 1-1 kwenye mechi hiyo iliyochezwa Jumatano usiku.

Seydou Doumbia alikuwa amewapa CSKA uongozi dakika ya 15, akiwa wa kwanza kufikia mpira baada ya kipa wa United David de Gea kutema penalti iliyochapwa na Roman Eremenko baada ya Martial kunawa mpira eneo la hatari.

United walitatizika kipindi cha kwanza lakini wakaimarika cha pili na Martial akaweza kulipia kosa lake kwa kufunga bao la kichwa kutoka kwa krosi ya Antonio Valencia.
Red Devils hao sasa wamo nambari mbili Kundi B baada ya Wolfsburg kulaza PSV Eindhoven na kutua kileleni.

Nahodha wa Manchester United Wayne Rooney alikuwa kimywa sana mechi hiyo, jambo ambalo si dalili njema ikizingatiwa kwamba wanasubiriwa na debi kali ya Manchester wikendi katika Ligi ya Premia.

Wapinzani wao wa Jumapili Manchester City walifunga bao la dakika za mwisho na kuandikisha ushindi wa 2-1 dhidi ya Sevilla katika mechi yao Ligi ya Klabu Bingwa iliyochezwa pia Jumatano usiku.

Hata hivyo, alama hiyo moja waliyojishindia United ugenini kwa CSKA Moscow inawawezesha kuendeleza matumaini kwenye kundi lao ambalo bado liko wazi.

Watakuwa katika nafasi nzuri iwapo wataweza kuwachapa viongozi hao wa ligi ya Urusi kwenye mechi ya marudiano uwanjani Old Trafford Novemba 3.

Yafuatayo ndiyo matokeo ya mechi zote za Uefa zilizochezwa Jumatano :

Paris St Germain 0 - 0 Real Madrid
CSKA Moscow 1 - 1 Manchester Utd
Manchester City 2 - 1 Sevilla
Malmö FF 1 - 0 Shaktar Donetsk
VfL Wolfsburg 2 - 0 PSV
Atletico Madrid 4 - 0 FC Astana

BBC

Changia hii habari na wenzako.

Comments

Tumia Comments